Klabu ya FC Barcelona imeendelea kujivunia hazina mpya ya vipaji kupitia akademi yake maarufu ya La Masia, baada ya kinda mwenye umri wa miaka 12, Fode Diallo, kuweka rekodi ya kipekee isiyotarajiwa.
‎Diallo, ambaye amezaliwa nchini Hispania akiwa na asili ya Guinea, ameandika historia kwa kufunga mabao 97 katika michezo 30 pekee kwenye ngazi ya vijana — rekodi inayomfanya kuwa mfungaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya La Masia.
Mafanikio hayo yamewavutia wengi barani Ulaya, huku yakivunja rekodi zilizowahi kuwekwa na nyota waliopitia akademi hiyo kama Takefusa Kubo, Lamine Yamal, Toni Fernández na Ansu Fati.
Katika tukio lililovutia hisia za mashabiki, Diallo alipata nafasi ya kukutana na Yamal na kupiga naye picha ya pamoja, ishara ya kizazi kinachong’ara sasa na kile kinachokuja kwa kasi kubwa siku zijazo.
Wakati Yamal tayari ameanza kung’ara kwenye soka la Ulaya, Diallo anaonekana kuwa nyota anayefuata, akiwa na ndoto na matumaini ya kuifikia mafanikio makubwa kupitia njia ile ile ya La Masia.
Hakika, hiki ni kizazi kipya kinachoibuka kwa kasi, kikibeba ndoto moja ndani ya akademi moja — kuuteka ulimwengu wa soka.




