Tuesday, December 16, 2025
spot_img
HomeHabariMatch Masters yashitaki Tanzania Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu ushuru wa viberiti

Match Masters yashitaki Tanzania Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu ushuru wa viberiti

Kampuni ya Match Masters Limited, mtengenezaji mkubwa zaidi wa viberiti salama Afrika Mashariki, imewasilisha kesi ya dharura katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) dhidi ya Serikali ya Tanzania, ikipinga ushuru mpya wa forodha uliowekwa kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2025.

Ushuru huo mpya, ambao unatoza Shilingi 400 kwa kilo ya viberiti vinavyoingizwa, umeelezwa na kampuni hiyo kuwa wa kibaguzi na kinyume na Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kwa mujibu wa Match Masters, ushuru huu unaathiri moja kwa moja ushindani huru wa kibiashara kwa kuondoa kodi kwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania huku ukiweka mzigo mkubwa kwa viberiti vinavyotoka Kenya na nchi nyingine za EAC.

Athari za ushuru huo zimeanza kujitokeza mara moja, ambapo bei ya viberiti imepanda kwa zaidi ya Shilingi 2,000 kwa katoni yenye boksi 1,000, hali inayowaumiza zaidi wananchi wa kipato cha chini.

Match Masters, inayojulikana kwa bidhaa zake maarufu Kasuku, Tinga na Paka ambazo hutumika katika kaya nyingi za Kitanzania, imesema hatua hiyo inaweza kuhatarisha mustakabali wake wa kibiashara na kuathiri maelfu ya watu walioko kwenye mtandao wake wa usambazaji na usafirishaji nchini.

Akizungumza baada ya kufungua kesi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Match Masters, Kushal Shah, alisema:

“Kwa miaka 23 tumekuwa tukiwapatia Watanzania viberiti vyenye ubora wa juu na bei nafuu. Tumeshangazwa na kusikitishwa kuona safari hii inaweza kufika mwisho kutokana na ushuru wa kibaguzi usio na sababu za wazi. Walioathirika zaidi ni wananchi wa kipato cha chini waliokuwa wakitegemea Kasuku, Tinga au Paka kwa mahitaji ya kila siku ya kuwasha majiko na moto.”

Shah alionya kuwa iwapo hatua hii haitarekebishwa, kampuni yake italazimika kupunguza kiwango cha uzalishaji, jambo litakalosababisha kupotea kwa ajira na mapato ya biashara nyingi zinazohusiana na bidhaa hizo.

Kampuni hiyo imejenga hoja zake kwa kuzingatia Ibara ya 75(4) na 75(6) ya Mkataba wa EAC, zinazokataza uanzishaji wa ushuru mpya kati ya nchi wanachama na kuzuia hatua za kibaguzi dhidi ya bidhaa kutoka ndani ya jumuiya.

Tayari, Shirikisho la Watengenezaji Bidhaa Kenya (KAM) limeungana na Match Masters kupinga kodi hiyo, likieleza kuwa sio tu inawaumiza wazalishaji wa Kenya, bali pia wazalishaji wote wa EAC wanaouza bidhaa zao nchini Tanzania.

Aidha, wachambuzi wa kibiashara wanasema kesi hii ni jaribio kubwa la kuangalia iwapo Tanzania inazingatia makubaliano ya kanda, ikizingatiwa kuwa Mahakama ya EACJ imewahi kutoa maamuzi yenye mfano kama ilivyokuwa katika kesi ya Kioo Limited dhidi ya Serikali ya Kenya mwaka 2020, kuhusu ushuru wa chupa za glasi.

Kwa sasa, macho ya wadau wa biashara na wananchi yameelekezwa kwa Mahakama ya EACJ, wakisubiri kuona kama itatoa uamuzi utakaolinda misingi ya soko la pamoja na kupunguza athari za kiuchumi zinazowakabili wananchi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments