Thursday, December 18, 2025
spot_img
HomeMichezoGamondi: Kwa Chama hizi ndio zake

Gamondi: Kwa Chama hizi ndio zake

Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Angel Gamondi, amesema hakuona ajabu yoyote kwa kile alichokifanya kiungo mshambuliaji Clatous Chama katika fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya Al Hilal ya Sudan, akisisitiza kuwa Mzambia huyo ni mchezaji wa mechi kubwa na maamuzi.

Chama alifunga mabao yote mawili dakika ya 20 na 57, na kuiwezesha Singida Black Stars kutwaa ubingwa wa Kagame Cup 2026 kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo, baada ya kuichapa Al Hilal 2–1 kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Gamondi alisema hakushangazwa na kiwango cha Chama kwa kuwa amekuwa akifanya makubwa kwenye klabu kubwa hapa nchini na katika mechi muhimu za kimataifa.

“Nina furaha kubwa baada ya kuchukua ubingwa huu, ambao ni ishara nzuri kuelekea msimu mpya wa ligi. Kuhusu Chama, sijashangazwa na alichokifanya. Nimemjua kama mchezaji mkubwa mwenye uwezo wa kurahisisha kazi eneo la ushambuliaji, iwe kwa kutoa pasi za mabao au kufunga mwenyewe. Haya ndiyo mambo yake katika mechi kubwa,” alisema raia huyo wa Argentina.

Aidha, Gamondi aliwajibu wanaomkosoa Chama kwa kigezo cha umri akisema soka halipimi umri bali kiwango na kazi inayofanyika uwanjani.

Kwa upande wake, Chama alisema ubingwa huo ulikuwa matokeo ya juhudi kubwa za timu nzima, kwani wapinzani wao Al Hilal ni klabu bora yenye uzoefu mkubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Hii ni timu kubwa, ilibidi tupambane kama kikosi kwa kila hali ili tushinde,” alisema Chama, akiongeza kuwa siri ya kiwango chake bora ni nidhamu na malengo binafsi.

Hata hivyo, alisema kikosi cha Singida bado hakijakaa vizuri na wanaendelea kujiandaa kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments