Mkurugenzi wa Huduma za Ubora wa Maji kutoka Wizara ya Maji, Mteki Chisute, amesema Tanzania ina zaidi ya mabwawa 700 ya maji na takribani 60 ya taka sumu, ambayo kwa tathmini ya sasa, yako katika hali nzuri ya usalama bila kuleta madhara kwa binadamu au mazingira.
Akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa Usalama wa Mabwawa 2025 uliofanyika jana jijini Mwanza, Chisute alisema mikutano ya kitaalamu ni muhimu kwa kujengeana uwezo, kupanga mipango ya kukabili hatari na kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza endapo kutatokea dosari kwenye mabwawa.
Ameeleza kuwa tayari kuna mikakati madhubuti ya kitaifa na kimataifa inayotekelezwa, ikihusisha mpango wa kukabiliana na hatari, ufuatiliaji wa karibu na tathmini endelevu katika maisha yote ya bwawa ili kugundua mapema vihatarishi na kuchukua hatua kwa wakati.
Chisute amesema licha ya faida nyingi za mabwawa kwa jamii, ni lazima wamiliki na wadau kuhakikisha mipango ya usimamizi na usalama inazingatiwa, hususan kwenye mabwawa ya taka sumu. Serikali pia imenunua mitambo mipya kwa uchimbaji na ujenzi wa mabwawa pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalam na wamiliki ili kuhakikisha usimamizi bora wa miradi.
Amebainisha kuwa mabwawa makubwa, ya kati na madogo yameendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za maji na kudhibiti taka sumu zisije kuathiri mazingira.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maji, mabwawa yote yanapaswa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji (Sura 331) na Kanuni za Usalama wa Mabwawa, jambo ambalo ni wajibu wa kisheria na kimaadili kwa ustawi wa jamii.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Wizara na Chama cha Wachimbaji Tanzania, kwa msaada wa City Engineering Company Ltd, umeongeza uwezo wa wamiliki wa mabwawa, washauri na wadhibiti kupitia matukio ya kitaalamu yaliyofanyika mwaka 2023 na 2024 kuhusu teknolojia mpya na usimamizi bora wa mabwawa.

Katika mkutano huo wa siku tatu, washiriki wanatarajiwa kupata maarifa mapya yatakayowaongezea ujasiri na uwezo wa kukabiliana na dharura zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Chamber of Minerals, alisema wachimbaji wote—wakubwa na wadogo—hufuata utaratibu wa kutathmini athari za mazingira kabla ya kuanzisha miradi, ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara kufuatilia mabwawa ya maji na taka sumu.
“Hakuna mgodi unaoruhusiwa kutiririsha maji yenye kemikali kwenye mazingira. Ikijitokeza nyufa au uvujaji, hatua za haraka huchukuliwa na mamlaka kama NEMC, Wizara ya Maji na Tume ya Madini,” alisema.
Naye Dk. Menan Jangu, Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira, alibainisha changamoto za kimazingira kwenye usimamizi wa mabwawa, ikiwemo kupungua kwa virutubisho maeneo ya chini ya mabwawa jambo linaloweza kuathiri kilimo, na madhara makubwa yanayoweza kutokea iwapo bwawa litabomoka.
“Kwenye mabwawa ya tope sumu, kutokuzingatia viwango kunaweza kusababisha sumu kuingia kwenye vyanzo vya maji au mashamba na kuathiri afya na mazingira,” aliongeza.
Kwa upande wake, Zonnastraal Mumbi, Mhandisi wa mgodi wa Barrick – Buzwagi, alisema kampuni hiyo imewekeza kwenye mifumo imara ya usalama wa mabwawa kwa kujenga miundombinu ya kutunza na kuhifadhi maji bila kuathiri mazingira.





