Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kupambana na maradhi, moja ya maadui wakuu watatu waliotajwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya serikali ya awamu ya sita, Hapi alisema kuwa Rais Samia amehakikisha Watanzania, mijini na vijijini, wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo wanayoishi.
“Baba wa Taifa aliwahi kusema kwamba tunao maadui wakubwa watatu: ujinga, umasikini, na maradhi. Yawezekana tuna maadui wengi, lakini hao ni wakubwa watatu. Sasa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi kubwa sana katika kupambana na adui maradhi,” alisema Hapi.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, ajenda yake kuu imekuwa kuboresha huduma za afya kwa Watanzania wote bila kujali maeneo wanayoishi, hatua ambayo imeleta maendeleo makubwa katika sekta ya afya nchini.