Na Getrude Mpezya.ARUSHA
Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe amezindua mitambo maalum ya kukarabati Barabara za mitaa 154 na malori mawili mapya.

Wakati wa uzinduzi huo,Iranqhe mbele ya Wananchi wa Jiji la Arusha ameelekeza Kila Kata kukabidhiwa shilingi Milioni 4, kwaajili ya manunuzi ya vifusi vya kujengea barabara hizo, ikiwa ni fedha baki kwenye bajeti ya Shilingi Bilioni 2 zilizokuwa zimetengwa awali kwenye manunuzi ya Mitambo ya ujenzi wa barabara hizo.
Katika hatua nyingine, Mstahiki meya pia amehimiza suala la utunzaji wa mazingira, akiwasihi madiwani kusimamia ajenda hiyo ya upandaji wa miti kwa wingi hasa katika maeneo yanayokumbwa na ukame huku pia akitahadharisha kuhusu ongezeko kubwa la utupaji wa taka mitaani hasa chupa za Plastiki zinazozagaa kwenye mitaro na maeneo mbalimbali ya wazi suala linalodumaza sifa ya Mkoa wa Arusha kuwa Kitovu cha Utalii kwa Tanzania bara.


Hata hivyo Mkurugenzi wa Jiji la Arusha John Kayombo kabla ya kumkaribisha amesema mitambo hiyo itakwenda kujenga na kukarabati barabara za mitaa yote 154, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa,Paul Makonda kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa kuhakikisha Arusha inanufaika na miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
