Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, CP Suzan Kaganda, ametembelea ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) zilizopo mjini Harare na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa TPA nchini humo, Kulthum Boma, kuhusu namna ya kuimarisha huduma na kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo kupitia bandari za Tanzania.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi, yenye lengo la kuendeleza mchango wa TPA katika kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandari za Tanzania kwenda nchi za Kusini mwa Afrika, ikiwemo Zimbabwe.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kulthum Boma alieleza kuwa ofisi hiyo yenye jukumu la masoko na huduma kwa wateja imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza shehena ya mizigo inayoingia Zimbabwe kupitia bandari za Tanzania tangu kufunguliwa kwake rasmi mwaka 2023.
Kwa upande wake, Balozi Kaganda amepongeza mafanikio hayo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya ofisi ya TPA na Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Aidha, ameshauri kuandaliwa kwa mikutano na wadau pamoja na wafanyabiashara nchini Zimbabwe ili kuongeza uelewa na kuhamasisha matumizi ya bandari za Tanzania, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa biashara na kuongeza pato la taifa.





