Benki ya Absa Tanzania, World Vision wakabidhi mradi wa maji kwa wakazi wa Kwedizinga

Benki ya Absa Tanzania kwa kushirikiana na shirika la World Vision Tanzania imekabidhi rasmi mradi wa kisima cha maji chenye pampu inayotumia nishati ya jua pamoja na mtandao wa usambazaji wa maji kwa wakazi wa Kijiji cha Kwedizinga, Wilaya ya Handeni.

Hafla ya makabidhiano ya mradi huo uliodhaminiwa na Benki ya Absa kwa gharama ya shilingi milioni 50 za Kitanzania, ilifanyika katika eneo la kisima hicho na kuhudhuriwa na viongozi kutoka RUWASA, serikali ya kijiji pamoja na wadau wengine. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Batilda Burian, aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese.

Akizungumza katika hafla hiyo, Aron Luhanga, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mahusiano ya Kibiashara wa Benki ya Absa Tanzania, alieleza dhumuni la mradi huo:
“Huu si mradi wa miundombinu tu, bali ni hadithi ya matumaini, ubinadamu na fursa. Kwa muda mrefu, upatikanaji wa maji salama umekuwa kikwazo kwa mustakabali wa watoto wa Kwedizinga. Leo tunatimiza dhamira yetu ya kuwawezesha Waafrika kwa ajili ya kesho bora… hadithi moja baada ya nyingine. Tunajivunia kuwa chachu ya maendeleo katika jamii hii, kwa sababu kwetu, hadithi ya kila Mtanzania ina thamani.”

Alisema kuwa mradi huo ulianza miezi michache iliyopita na sasa umewezesha wakazi zaidi ya 3,800 kutoka vitongoji saba kupata maji safi kwa uhakika. Hapo awali, jamii hiyo ilitegemea mabwawa ya msimu ambayo hukauka wakati wa kiangazi, na hivyo kulazimisha wanawake na watoto kutembea zaidi ya kilomita mbili kila siku kutafuta maji yasiyo salama.

“Kisima hiki kina urefu wa mita 180 na kinatumia pampu inayotumia umeme wa jua. Maji yanahifadhiwa katika tanki la juu lenye ujazo wa lita 50,000 na kusambazwa kwa mfumo wa mvuto. Mtandao huu unajumuisha mabomba na vituo 10 vya kuchotea maji vilivyotawanyika katika kijiji,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, James Anditi alisema:
“Shauku yetu kuu kama World Vision Tanzania ni kuona kila mtoto anastawi na kuishi maisha yenye matumaini na fursa. Maji safi si mahitaji ya msingi tu, bali ni msingi wa ulinzi wa mtoto, afya, elimu na uthabiti wa kiuchumi. Mradi huu, ambao ni sehemu ya mkakati wetu wa Maji, Usafi na Mazingira (WASH), unaakisi maono hayo kwa kuleta mazingira salama na yenye afya kwa watoto kustawi.”

Aliongeza kuwa:
“Tunatoa shukrani za dhati kwa Benki ya Absa kwa kushirikiana nasi kuhakikisha kuwa watoto wa Kwedizinga sasa wanatumia muda mwingi darasani badala ya kuchota maji, na familia zao zinalindwa dhidi ya magonjwa yanayozuilika kama kuhara na homa ya matumbo. Huu ni mfano wa athari chanya na ya kudumu tunayolenga kuipeleka kwenye jamii.”

Mgeni rasmi wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Burian, alisema mradi huo ni mfano wa mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma katika kutatua changamoto za kijamii.

“Mradi huu unaonesha kuwa kwa malengo ya pamoja, tunaweza kutatua hata changamoto kubwa zaidi katika jamii zetu. Nawapongeza kwa dhati Benki ya Absa na World Vision kwa kuwa mfano wa kuigwa kitaifa,” alisema.

Mradi huu unachangia moja kwa moja Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) Awamu ya Tatu na unaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hususan SDG 3 (Afya Bora na Ustawi), SDG 4 (Elimu Bora) na SDG 6 (Maji Safi na Usafi wa Mazingira).

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *