CCM na mageuzi ya kidigitali chini ya uenyekiti wa Dkt. Samia

Kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwake mwaka 1977, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeandika ukurasa mpya katika historia ya siasa za Tanzania, kwa kufanya Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa kwa njia ya kidijitali.

Hatua hii haikuja kwa bahati mbaya. Ni matokeo ya mabadiliko ya kimfumo, kifikra na kiteknolojia yanayoendelea chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mkono wake, chama kimeingia rasmi katika zama za kisasa kwa kuingiza vipengele vya mikutano ya mtandaoni kwenye Katiba yake, kupitia marekebisho madogo ya Mei 2025, chini ya Ibara ya 99(3).

Huu si uamuzi wa kawaida, ni ujasiri wa kisiasa unaobeba sura ya kiongozi aliyeamua kupeleka chama mbele ya wakati.Kwa mtu anayeifuatilia historia ya vyama vya siasa duniani, hii si ajabu. Vyama vikongwe kama Liberal International tayari vimewahi kufanya mikutano kwa njia ya mtandao.

Nchini Italia, chama cha Five Star Movement kilijipambanua kwa mfumo wake wa Rousseau, ambapo wanachama waliamua sera na viongozi kupitia kura za mtandaoni.

Kwa CCM, chama kilichobeba historia ya ukombozi, sasa kinabeba pia mustakabali wa mageuzi ya kisasa.

Katika zama ambazo teknolojia imeshika hatamu, hatua ya CCM si tu ya kisasa, bali ya kimkakati pia.

Kwa kutumia mtandao, chama kinapunguza gharama za mikutano mikubwa, kinapanua wigo wa ushiriki kutoka ngazi ya chini hadi taifa na kuongeza uwazi kwa wanachama wake.

Hii ni siasa ya karne ya 21 isiyohitaji mahema wala tiketi za ndege, kinachohitajika ni fikra hai, mfumo madhubuti na uamuzi thabiti wa kisiasa.

Yote hayo yako katika maoni ya Dkt. Samia.Kwa hakika, Dkt. Samia anazidi kuudhihirishia umma kuwa ni kinara wa mageuzi ndani ya CCM.

Amefanya mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri, amesimamia ajenda ya maendeleo jumuishi, na sasa anakisuka chama chake kuwa taasisi inayoweza kushindana na vyama vingine duniani kwa kutumia teknolojia.

Wapo watakaosema huu ni ‘ujanja wa kisasa’, lakini kwa muktadha wa sasa, huu ni ushahidi kuwa CCM haijaishiwa pumzi.

Inapumua, inatembea na sasa inazungumza kidijitali.Hii si CCM ya jana tu. Hii ni CCM ya kesho. Na kesho hiyo ina sura ya mwanamke jasiri, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *