Chalamanda ajiunga na JKT kuchukua mikoba ya Yacoub

Klabu ya JKT Tanzania imemsajili rasmi kipa wa zamani wa Kagera Sugar, Ramadhani Chalamanda, kuchukua nafasi ya Yacoub Suleiman, ambaye anatajwa kuhamia Simba SC.

Chalamanda, aliyesaini mkataba wa miaka miwili, amesifiwa kwa uwezo wake licha ya timu yake kushuka daraja. Anatajwa kuwa miongoni mwa makipa waliookoa michomo mingi na penalti katika msimu uliopita.

“Tulizingatia uwezo wake binafsi. Alikuwa na ‘saves’ nyingi, na ameonyesha umahiri mkubwa licha ya mazingira ya timu yake,” kilisema chanzo kutoka JKT.

Kipa huyo alisema yuko tayari kuichezea timu yoyote inayokubaliana naye kwenye maslahi, kwani kazi yake ni kucheza soka.

Usajili huu ni sehemu ya maboresho ya kikosi cha JKT, baada ya baadhi ya wachezaji wao akiwemo Yacoub, Wilson Nangu na Karim Mfaume kuhusishwa kujiunga na Simba SC.

JKT ilimaliza msimu uliopita nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu, ikiwa na alama 36, na kuweka rekodi ya kutoa sare nyingi kwa misimu miwili mfululizo — sare 12 msimu huu na sare 14 msimu wa 2023/24.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *