Chuo cha Kodi (ITA) kimetangaza mkakati wake wa kuimarisha mafunzo kwa kutumia teknolojia za kisasa za kidijitali ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani. Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Isaya Jairo, wakati akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya mahafali ya 18 ya chuo hicho yatakayofanyika kesho.
Profesa Jairo amesema kuwa kwa sasa chuo kinajivunia mafanikio ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano, ambao umeweka kipaumbele kwenye mafunzo kwa njia ya kiteknolojia pamoja na utekelezaji wa mpango wa mafunzo ya lazima kwa watumishi wapya na waliopo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Aidha, amesema chuo kimeendelea kufaidika na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na vyuo rafiki vya ndani na nje ya nchi, hali inayoongeza ubora wa elimu inayotolewa.
“Mafunzo kwa teknolojia ya kisasa ya kidijitali yatakisaidia chuo chetu kutoa elimu bora inayoendana na maendeleo ya kiteknolojia duniani,” alisema Profesa Jairo.
Katika mahafali hayo, Balozi Hamis Mussa Omar, Waziri wa Fedha, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na atawatunuku vyeti, stashahada, shahada na stashahada ya uzamili kwa jumla ya wahitimu 561 wa mwaka wa masomo 2024/2025. Kati yao, 317 ni wanaume na 244 ni wanawake.
Profesa Jairo alifafanua mgawanyo wa wahitimu kama ifuatavyo:
- 256 watatunukiwa Cheti cha Uwakala wa Forodha cha Afrika Mashariki (EACFFPC)
- 47 watatunukiwa Cheti cha Usimamizi wa Forodha na Kodi
- 26 watatunukiwa Stashahada ya Usimamizi wa Kodi
- 214 watatunukiwa Shahada ya Usimamizi wa Forodha na Kodi
- 18 watatunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Kodi
Ameongeza kuwa mwaka huu kumekuwa na ongezeko la wahitimu 144, kutoka 417 hadi 561, ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 ambalo linaonesha ukuaji wa uhitaji wa mafunzo ya kodi nchini.




