Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kwa kushirikiana na Serikali, imefanikiwa kuwekeza Trilioni 1.19 katika utekelezaji wa miradi ya majisafi ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya miradi na huduma, alisema kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 796.19 zimetumika kwenye miradi ya majisafi, huku Bilioni 400.91 zikitumika kwenye miradi ya usafi wa mazingira.
Miradi Iliyokamilika na Inayoendelea
Mhandisi Bwire alieleza kuwa miradi yenye thamani ya Bilioni 344.67 imekamilika, ambapo Bilioni 329.97 zilitumika kwenye miradi ya majisafi, huku Bilioni 14.7 zikitumika kwenye miradi ya usafi wa mazingira.
Aidha, miradi inayoendelea kutekelezwa ina thamani ya Bilioni 852.43, ambapo miradi ya majisafi ina thamani ya Bilioni 466.22 na ile ya usafi wa mazingira ina thamani ya Bilioni 386.21.
Miradi Mikubwa ya Maji Iliyokamilika
1. Mradi wa Maji Chalinze Awamu ya Tatu
Mradi huu umejengwa kwa lengo la kusambaza maji kwa wakazi wa Chalinze, Mboga, Msoga, na Miono. Umehusisha:
- Ujenzi wa vituo vitatu vya kusukuma maji (Miono, Msoga, na Mboga).
- Ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 923.
- Ujenzi wa matenki 18 ya maji yenye uwezo wa kuhifadhi kati ya lita 500,000 hadi milioni 2.
- Ujenzi wa vioski 330 vya kuchotea maji.
Mradi huu unanufaisha wakazi 400,000 wa Miono, Vigwaza, Lugoba, Ubena-Zomozi, Gwata, Mkata, Ngerengere, Manga, Mbwewe, na Fukayosi.
2. Mradi wa Maji Mlandizi – Chalinze – Mboga
Mradi huu umekamilika mwaka 2021 na umenufaisha zaidi ya wakazi 125,000 katika maeneo ya:
- Viwanda vya Twyford, Kiwanda cha Ngozi, na Kiwanda cha Juice Sayona.
- Stesheni ya Treni ya Mwendokasi.
- Vigwaza, Mboga, Chamakweza, Chahua-Lukenge, Milo, Ruvu Darajani, Mdaula-Ubena Zomozi, Buyuni, Visezi, Pingo, Pera, Bwilingu, Chalinze Mjini, Chalinze Mzee, na Soga.
Gharama ya utekelezaji wa mradi huu ni Bilioni 19.89.
3. Mradi wa Maji Makongo – Bagamoyo
Mradi huu umetekelezwa kwa gharama ya Bilioni 77.9 na umehusisha:
- Ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 1,252.
- Ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa lita milioni 5.
- Kuunganisha wateja wapya 40,000.
Mradi huu unanufaisha wakazi wapatao 450,000 wa Bagamoyo, Mapinga, Mbweni, Bunju, Wazo, Tegeta A, Salasala, Goba, Mabwepande, na Mivumoni.
4. Mradi wa Maji Mshikamano
Mradi huu umekamilika kwa asilimia 100, ukiwa umegharimu Bilioni 4.8 na umehusisha:
- Ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye lita milioni 6.
- Ujenzi wa kituo cha kusukuma maji.
Wananchi zaidi ya 180,000 wa Mshikamano, Msakuzi, Machimbo, na Majengo Mapya wamenufaika na mradi huu.
5. Mradi wa Maji Kigamboni
Mradi huu umehusisha:
- Ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji lenye uwezo wa lita milioni 15.
- Ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 6.35.
Zaidi ya wakazi 450,000 wa Kigamboni wananufaika na kukamilika kwa mradi huu.
Ongezeko la Uwezo wa Uzalishaji na Usambazaji wa Maji
Kutokana na utekelezaji wa miradi hii, uwezo wa uzalishaji wa maji umeongezeka kutoka lita milioni 500 kwa siku hadi lita milioni 534 kwa siku, sawa na ongezeko la lita milioni 34.1.
Chanzo cha ongezeko hili ni:
- Mtambo wa Wami (lita milioni 14.1 kwa siku).
- Visima vya Kimbiji (lita milioni 20 kwa siku).
Aidha, mtandao wa usafirishaji na usambazaji maji umeongezeka kutoka kilomita 4,690.7 hadi kilomita 7,206, sawa na ongezeko la kilomita 2,513.4.
Ongezeko la Uwezo wa Kuhifadhi Maji
Mhandisi Bwire alieleza kuwa uwezo wa kuhifadhi maji umeongezeka kutoka lita milioni 153.6 hadi lita milioni 198.9, sawa na ongezeko la lita milioni 45.3. Maji haya yanahifadhiwa kwenye matenki ya:
- Vikawe
- Tegeta A
- Mshikamano
- Mbweni
- Bangulo
- Kigamboni
Ongezeko la Wateja wa Majisafi
Idadi ya wateja wa huduma ya majisafi imeongezeka kutoka 343,019 hadi 455,720, sawa na ongezeko la wateja 112,701.
Kutokana na juhudi hizi, kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi kimepanda kutoka asilimia 89 hadi asilimia 93.
Mpango wa DAWASA Kuongeza Upatikanaji wa Majisafi
Mhandisi Bwire alisisitiza kuwa DAWASA inaendelea na juhudi mbalimbali kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya majisafi. Lengo ni kufanikisha azma ya serikali ya kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.
