Taasisi ya CRDB Bank Foundation imesema imepokea jumla ya maombi 3,967 kutoka kwa vijana wajasiriamali waliojitokeza kuomba uwezeshaji kupitia mradi wake wa Go Green na IMBEJU uliozinduliwa tarehe 12 mwezi uliopita.
Matokeo hayo yametangazwa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa akifunga dirisha hilo la maombi na kueleza kuwa hatua inayofuata sasa ni kufanya tathimini ya kiufundi itakayozingatia ubunifu wa wazo la biashara, uendelevu wa mradi, uwezo wa biashara kujiendesha pamoja na mchango wake katika kulinda mazingira.
“Mchakato huu utakamilika ndani ya wiki moja. Hatua ya tatu itakuwa kuhakiki biashara zinazofanya kazi kuona kama kweli zinaendana na mawasilisho yao. Zoezi hili litachukua takribani wiki tatu kwani biashara zote zitatembelewa kuona uhalisia wake kabla ya kutangaza biashara zilizokidhi vigezo vya kupata mtaji wezeshi ambao ni kati ya shilingi 500,000 na shilingi milioni 500,” amesema TullyEsther.




Tathmini ya maombi yaliyopokelewa itafanywa na jopo la wataalamu kutoka CRDB Bank Foundation, Benki ya CRDB, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Tume ya TEHAMA (ICTC) na Wizara ya Maendeleo ya Vijana pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia Mazingira.
Kupitia Go Green na IMBEJU, CRDB Bank Foundation inakusudia kuwawezesha vijana wanaomiliki kampuni changa, wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wakiwemo ambao biashara zao hazijarasimishwa pamoja na wanafunzi waliopo vyuoni wenye mawazo ya biashara ambayo yanaweza kugeuzwa kuwa biashara halisi.

Sifa muhimu kwa makundi yote matatu ni kuwa na ubunifu au biashara zenye uelekeo wa uchumi wa kijani kama vile kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, uvuvi, matumizi ya nishati safi na jadidifu, teknolojia za maji na umwagiliaji, usimamizi wa taka na mazingira, pamoja na ubunifu wa kidijitali unaosaidia kulinda mazingira na kuboresha uzalishaji.
Kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wametuma mawazo yanayoweza kubidhaishwa, watapewa kati ya shilingi 500,000 na shilingi milioni 10 kuwasaidia kuyatekeleza ili kushiriki kutatua changamoto zilizopo katika jamii.








