Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk. Dotto Biteko, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Nzega kwa kuwa mfano bora katika udhibiti wa upotevu wa maji, baada ya kufanikisha kiwango cha chini cha upotevu wa asilimia 6 pekee.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutangaza tathmini ya utendaji wa mamlaka mbalimbali za maji kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Dk. Biteko alizitaka mamlaka nyingine nchini kuiga mfano wa Nzega ili kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu inatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.
“Upotevu wa maji ni changamoto kubwa inayosababisha hasara kwa mamlaka za maji na wananchi kwa ujumla. Nzega imeonesha mfano mzuri wa udhibiti wa upotevu wa maji, na mamlaka nyingine zinapaswa kujifunza kutoka kwao ili kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Dk. Biteko.
Hata hivyo Dk. Biteko alisema pamoja na jitihada zinazoendelea jamii ina wajibu wa kuhakikisha usafi wa mazingira, kupanda miti na kuhifadi misitu ili kuendelea kupata na kutumia rasilimali maji.

“Tusipotunza vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira tutajikuta katika mtanziko mkubwa (water stress),” alisema na kuongeza kukosekana kwa rasilimali maji kwa baadhi ya watu kinaweza kuwa chanzo cha migogoro na machafuko katika jamii husika. Ili kukabilikana na hali hiyo na kumwezesha kila Mtanzania kupata huduma za maji na usafi wa mazingira, Dkt. Biteko amezielekeza mamlaka za maji kupunguza kiwango cha upotevu maji ili kuepusha hasara ya shilingi bilioni 114.12 iliyotokana na upotevu huo kwa mwaka huu.
Hadi sasa asilimia 84 kwa mijini na asilimia 79.6 kwa maeneo ya vijijini zimeunganishwa na huduma ya maji ambapo kuna ongezeko la asilimia 7 kutoka kipindi cha mwaka uliotangulia.
Awali, Waziri wa Maji, Juma Aweso alisema kumekuwa na ongezeko la ubora wa viwango vya maji na udhibiti wa upotevu wa maji ambao unasababisha hasara kubwa hasa unapothamanishwa kifedha.
Mbali na mafanikio hayo katika udhibiti wa upotevu wa maji, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Nzega pia imeibuka mshindi wa kwanza kwa mara ya tatu mfululizo katika utoaji wa huduma bora za majisafi na usafi wa mazingira kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Mamlaka hiyo ni miongoni mwa taasisi 18 zinazohudumia wateja kati ya 5,000 na 20,000, na ushindi huu ni uthibitisho wa utendaji wake bora.
Tuzo hiyo inaonesha dhamira ya mamlaka hiyo katika kuhakikisha huduma za maji zinatolewa kwa viwango vya juu huku ikizingatia uhifadhi wa mazingira na matumizi sahihi ya rasilimali maji.
