Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, ameongoza Ujumbe wa Tanzania katika kikao cha mashauriano ya ndani kuelekea katika Mkutano wa Kwanza wa Dharura wa Baraza la Kisekta la Mawaziri Wanaosimamia Masuala ya Fedha na Uchumi (SCFEA) wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaofanyika leo tarehe 25 Julai 2025, Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, jijini Arusha.

Mkutano huo ambao umehudhuriwa pia na wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wakiwemo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki), Dennis Londo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban, utajadili pamoja na mambo mengine, hatua za kikodi zilizo kwenye sheria za fedha za nchi wanachama zenye kuleta athari za kubagua bidhaa zilizozalishwa ndani ya nchi za Jumuiya.
Hatua hii ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano wa 46 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) na makubaliano ya Mawaziri wa Fedha wakati wa mashauriano ya kibajeti katika mikutano yao iliyofanyika mwezi Mei 2025.
