Dk. Samia aweka rekodi mpya CCM

Katika historia ya siasa za Tanzania, Julai 26, 2025 inabaki kuwa siku ya kipekee. Siku ambayo Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliandika ukurasa mpya wa mageuzi kwa kufanya Mkutano Mkuu wa Taifa kwa njia ya kidijitali, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwa chama hicho mwaka 1977.

Lakini zaidi ya teknolojia, historia hii imewekwa chini ya uenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha kuwa ni kiongozi mwenye usikivu kwa wanachama, maono ya mageuzi na mtetezi wa usawa na demokrasia ya kweli ndani ya chama.

Baada ya kukamilika kwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea ubunge na udiwani ndani ya CCM, ziliibuka kelele kutoka kwa wanachama wengine wakilalamikia muundo mpya wa uteuzi. Mfumo huu, uliopitishwa na Mkutano Mkuu wa Januari 2025, uliipa Kamati Kuu (CC) ya chama mamlaka ya kuchakata majina matatu ya wagombea yaliyopendekezwa na kamati za siasa za wilaya au mikoa.

Ingawa mfumo huo ulikuwa wa kikatiba, ulikosolewa kwa kuonekana kuwa unaweza kuwanyima fursa wagombea wengine waliokuwa na sifa, lakini hawakuwamo kwenye orodha hiyo fupi ya majina matatu.

Katika hali ya kawaida, chama kingeweza kusonga mbele kwa kuzingatia katiba kama ilivyo. Lakini hapa ndipo tofauti ya uongozi wa Dkt. Samia inapoonekana wazi. Badala ya kufunika kilio cha wanachama, alikitazama kwa jicho la busara, akakisikiliza kwa moyo wa mama, na akasogeza mbele tarehe ya uteuzi ili kupisha mchakato mpana zaidi wa kusikilizana.

Katika hatua ya kushangaza na ya kipekee, Dkt. Samia aliitisha Mkutano Mkuu wa Taifa kwa njia ya mtandao, lengo likiwa ni kuwashirikisha wajumbe kupitisha mabadiliko madogo ya Katiba ya CCM kwa njia salama, ya haraka na ya kisasa.

Kupitia mkutano huo wa kihistoria, wajumbe walitakiwa kuidhinisha mabadiliko yatakayoiwezesha Kamati Kuu kupokea majina zaidi ya matatu ya wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge, hasa pale panapokuwa na idadi kubwa ya watiania wenye sifa zinazofanana.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa mkutano huo wa kihistoria, Dkt. Samia alisema kwa sauti ya utulivu lakini yenye mshiko:

“Kuna maeneo kuna wagombea hadi 39 au 40. Tumeona kwenda na watatu kati ya watu wengi hao si jambo la busara. Lakini papo hapo Kamati Kuu imebanwa na Katiba, hatuwezi kuongeza majina… Tumeamua kurudi kwenu, kuomba ridhaa ya kubadilisha Katiba, kuongeza maneno, kama Kamati Kuu itakavyoona inafaa.”

Na wajumbe walimwelewa. Kwa kauli moja, wakapitisha mabadiliko hayo kwa asilimia 99.8, ikiwa ni dalili ya ridhaa pana na imani kwa uongozi wake.

Hatua hii haikuja kwa bahati mbaya. Tangu aanze kuiongoza CCM na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia ameongoza kwa mwamvuli wa falsafa ya 4R, Reconciliation (maridhiano), Resilience (ustahimilivu), Reforms (mageuzi), na Rebuilding (kujenga upya). Hili ni mojawapo ya matunda ya wazi ya falsafa hiyo.

Kwa kuweka msingi wa mashauriano, uamuzi huu haujajenga tu heshima kwa Katiba ya chama, bali umeonyesha kwa vitendo kuwa ndani ya CCM, sauti ya mwanachama mmoja mmoja ina uzito wake.

Katika mazingira ambayo vyama vingine bado vinakumbwa na migogoro ya ndani ya uteuzi na kulalamikiwa kwa neti zisizotoboka, CCM kupitia uongozi wa Dkt. Samia imedhihirisha ukomavu wake wa kisiasa kwa kufungua milango zaidi ya ushindani na ushirikishwaji.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia Julai 2025, zaidi ya wagombea 16,000 walijitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi za udiwani, huku zaidi ya 1,300 wakichukua fomu za ubunge. Kwa wingi huo, ni wazi kuwa orodha ya majina matatu ilikuwa haitoshi kutoa mwanya wa haki kwa wote.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *