Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la wavuvi la kulitumia lililokuwa jengo la abiria katika eneo la Kigongo, mkoani Mwanza, kuwa soko la samaki.
Awali, jengo hilo, lilitumika na abiria waliokuwa wanasubiri huduma ya vivuko, lakini sasa Serikali ya Dkt Samia imetekeleza mradi wa Daraja la JP Magufuli na hivyo kivuko hakitumiki tena.
Dk Samia ameridhia ombi hilo leo, Jumanne Oktoba 7, 2025 alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, katika mkutano wake wa kampeni za urais.
“Kwa hatua ya sasa sidhani kama kuna kizuizi chochote kwenye kuzuia jengo hilo, nadhani halmashauri ilichukue na kufanyia kazi,” amesema.
Pamoja na kuridhia ombi hilo, ameahidi kujenga soko jipya la samaki na kama eneo ni lile lile la Busisi, litarekebishwa kwa kuwekwa vifaa vya kuhifadhia samaki.