Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, anatarajiwa kufanya ziara ya siku tano katika majimbo ya Tunduru Kusini, Tandahimba, Mtwara Mjini, Lindi Mjini na Kilwa Kusini kuanzia Januari 05 hadi 09, mwaka huu.
Ziara hiyo ni ya kwanza kwa kiongozi huyo tangu kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Katika ziara hiyo, Dorothy Semu atakutana na viongozi wa Chama ngazi za mikoa na majimbo pamoja na waliokuwa wagombea wa ubunge na udiwani, kwa lengo la kusikiliza maoni yao, kufanya tathmini ya uchaguzi na kutoa ufafanuzi kuhusu misimamo mbalimbali iliyochukuliwa na Chama baada ya uchaguzi huo.
Aidha, ziara ya Kiongozi wa Chama inatarajiwa kufuatiwa na ziara nyingine za viongozi wakuu wa ACT Wazalendo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano wa chama na kuendelea na majadiliano ya ndani baada ya uchaguzi.




