*Mwamuzi Issa Sy awa gumzo, alitoa kadi nyekundu mfukoni kaishikilia
Klabu ya Esperance de Tunis imefanikiwa kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ahly katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), uliopigwa usiku wa kuamkia leo katika dimba la Hammadi Agrebi, Tunisia.
Bao pekee la mchezo lilifungwa dakika ya 73 kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na beki Mohamed Amine Tougai. Penalti hiyo ilitolewa baada ya beki wa Ahly, Mohamed Hany, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. Awali mwamuzi hakuliona tukio hilo, lakini baada ya msaada wa teknolojia ya VAR alimuita na kumruhusu kulipitia tukio hilo upya kabla ya kuamua kutoa penalti.
Baada ya mchezo kumalizika, mwamuzi Issa Sy alionekana kushika kadi nyekundu huku wachezaji na benchi la ufundi la Ahly wakionyesha kutoridhishwa na maamuzi ya penalti. Hata hivyo, walijizuia kumzonga mwamuzi huyo walipoona tayari ameshika kadi nyekundu mkononi.

Mchezo wa marudiano unatarajiwa kupigwa Machi 22, 2026 nchini Misri katika dimba la Cairo International Stadium. Katika mechi hiyo, Ahly haitakuwa na mashabiki wake uwanjani kutokana na adhabu waliyopewa katika hatua ya makundi baada ya mashabiki wao kufungiwa kuhudhuria michezo miwili.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa Mei 25, 2024 katika mchezo wa mkondo wa pili wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Ahly iliibuka na ushindi wa 1-0 baada ya Roger Aholou wa Esperance kujifunga dakika ya nne ya mchezo.
Licha ya Esperance kuonekana kusuasua katika hatua ya makundi ya michuano hiyo, katika hatua hii ya robo fainali timu hiyo imeonyesha kiwango cha juu na kucheza kwa kujiamini kama mabingwa.
Kwa muda mrefu, michezo kati ya Esperance na Ahly imekuwa na ushindani mkali kiasi cha kuonekana kama vita ya soka barani Afrika.





