Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme nchini (ETDCO) imeibuka mshindi katika kipengele cha Mkandarasi Bora wa Ujenzi wa Miundombinu ya Umeme katika Tuzo za Zanzibar International Construction Awards (ZICA) zilizofanyika Februari 22, 2025, Zanzibar.

Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo kwa washindi, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema sekta ya ujenzi ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Aliwahimiza washiriki kutumia tuzo hizo kama chachu ya kufanya kazi kwa bidii ili kufikia viwango vya juu na kuleta tija kwa Taifa.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, CPA Sadock Mugendi, aliishukuru ZICA kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya umeme. Aliahidi kuendelea kutoa huduma zenye viwango vya juu ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.
“ETDCO tumejipanga kuboresha matumizi ya teknolojia kwa kununua mashine za kisasa na kuwajengea uwezo wataalamu wetu ili kufikia viwango vya kimataifa,” alisema CPA Mugendi.


Aliongeza kuwa ETDCO ina jukumu la kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo TANESCO, REA, na makampuni binafsi.
Tuzo za ZICA 2025 zilishirikisha jumla ya washiriki 150, ambapo ETDCO ilikuwa miongoni mwa washindi 30 waliotunukiwa tuzo kwa ufanisi wao katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme. Kampuni hiyo imepongezwa kwa juhudi zake za kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika, hatua inayochangia kukuza maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
