Mwanza, Agosti 4, 2025
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanzania, likiwemo suala la kujikwamua kiuchumi, kutumia nishati safi ya kupikia, na kuwekeza katika vituo vya mafuta vijijini.

Wito huo umetolewa na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina, wakati wa Maonesho ya Wakulima ya Nanenane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza.
Mhina amesema EWURA inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya nishati na maji, akisisitiza kuwa wananchi wa Kanda ya Ziwa wanayo nafasi kubwa ya kushiriki katika miradi ya kimkakati, ikiwemo ule wa bomba la mafuta unaopita katika mikoa ya Kagera na Geita.
“Sisi EWURA ndiyo tunasimamia ushirikishwaji wa wazawa katika mradi huu. Ili mtu aweze kushiriki ni lazima ajisajili katika kanzi data yetu. Kupitia maonesho haya, tunawapa elimu wananchi kuhusu namna wanavyoweza kunufaika, huku pia tukiendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia,” alisema Mhina.
Ameeleza kuwa dhamira ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaongezeka kutoka hali ya sasa hadi kufikia asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034.
Uwekezaji vijijini
Akizungumzia fursa za kiuchumi katika maeneo ya vijijini, Mhina amesema hadi sasa kuna zaidi ya vituo 500 vya mafuta vijijini nchini, lakini kiwango hicho bado ni kidogo, hasa kwa Mkoa wa Mwanza. Aliwahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kwa kuwekeza, akieleza kuwa EWURA imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wapya.

“Kwa sasa, mtu anaweza kuwekeza katika kituo cha mafuta vijijini kwa mtaji wa kuanzia Shilingi milioni 50. Tunatoa leseni na kusimamia shughuli hizo, na tumeweka masharti rahisi ili kuwavutia wawekezaji,” alifafanua.
Aidha, aliwataka wananchi wa Kanda ya Ziwa, ambao wengi ni wakulima na wafugaji, kutumia mitaji wanayopata kutokana na shughuli zao kuwekeza katika sekta ya mafuta na nishati.
Elimu kwa wananchi
Mhina pia aliwahimiza wananchi kutembelea banda la EWURA katika maonesho hayo ili kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali za sekta ya nishati na maji, ikiwa ni pamoja na gesi, umeme, na taratibu sahihi za kufunga miundombinu ya umeme.
“Tunawahimiza wananchi kufahamu mafundi waliosajiliwa rasmi na EWURA ili kuhakikisha usalama wa miundombinu ya umeme kwenye majengo yao, iwe ni mabanda ya mifugo, viwanda, au makazi ya kawaida,” alisisitiza.
Maonesho ya Nanenane yanaendelea kufanyika kwa wiki nzima yakilenga kuhamasisha shughuli za kilimo, mifugo, viwanda, na uwekezaji vijijini kupitia sekta mbalimbali.