Faida tano marekebisho ya Katiba ya CCM

Katika hali ya kisiasa inayobadilika kila uchao, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kuonyesha uhai na uwezo wa kujiimarisha kwa kufanya marekebisho yenye tija kwenye Katiba yake.

Miongoni mwa marekebisho yaliyozua mijadala chanya ni mabadiliko ya Ibara ya 99(3)(f) ya Katiba ya CCM, ambayo sasa yanaruhusu Kamati Kuu ya CCM (CCM) kurudisha majina ya watiania wa ubunge, wakilishi zaidi ya matatu yakapigiwe kura za maoni kwa kadri itakavyoona inafaa.

Hili ni jambo dogo kwa macho ya kawaida, lakini ni la msingi katika kuboresha mchakato wa uteuzi wa viongozi ndani ya chama na hatimaye kuimarisha demokrasia ya ndani kwa ndani.

Faida kuu tano zinazoibuka kutokana na mabadiliko haya ni dhahiri na bila shaka ni ushahidi wa uongozi makini wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyeendela kukiongoza chama kwa weledi, usikivu na msukumo wa mageuzi.

Kuongeza wigo wa uamuzi

Awali, Kamati Kuu ililazimika kuwasilisha majina matatu tu kwa wajumbe yakapigiwe kura za maoni. Hii ilimaanisha kwamba endapo kuna wagombea bora zaidi ya watatu, CC haikuwa na uwezo wa kuwachuja au kuwaona.

Kwa kuruhusu majina zaidi ya matatu, CC sasa ina nafasi ya kufanya uamuzi mpana na wenye mantiki kwa kuzingatia uwezo, rekodi, jinsia na usawa wa kanda.

Kwa mfano, katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2019, taarifa ya TAMISEMI ilionyesha kwamba asilimia 72 ya wagombea walikuwa wanaume. Kupitia marekebisho haya, CCM sasa inaweza kusaidia kuongeza ushiriki wa wanawake kwa kuwapa nafasi zaidi kupenya kwenye hatua ya NEC, hii ni katika muendelezo wa dhamira ya Dkt. Samia kuimarisha usawa wa kijinsia katika uongozi.

Kuzuia mianya ya rushwa na upendeleo

Mchakato wa majina matatu uliwahi kuwa na changamoto ya kupenyeza siasa za makundi, ushawishi wa fedha na upendeleo binafsi. Kwa kupanua idadi ya majina, nafasi ya mtu kununua au ‘kupenyeza’ jina lake pekee inapungua.

Kamati Kuu inakuwa huru kuchambua kwa kutumia hoja, si kwa kushinikizwa. Hili linaendana na dhamira ya Dkt. Samia ya kupambana na rushwa na kuboresha misingi ya uwajibikaji ndani ya chama.

Kuakisi utawala shirikishi na usikivu wa Dkt. Samia

Uamuzi huu unaonesha kwa vitendo dhamira ya Mwenyekiti Dkt. Samia kusikiliza maoni ya wanachama na kuyafanyia kazi. Katika hotuba yake ya Julai 27, 2024, wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa uteuzi wa wagombea wa CCM, alisisitiza: “Chama chetu kisikie kilio cha wanachama, tusonge mbele kwa kufanya mageuzi yenye kujenga.” Marekebisho haya ni kielelezo cha usikivu huo.

Kutoa nafasi kwa viongozi wenye uwezo

Katika historia ya siasa za CCM, wapo wagombea waliokatwa mapema licha ya kuwa na uwezo mkubwa kwa sababu ya kikomo cha majina matatu.

Mabadiliko haya yanaruhusu vipaji visivyokuwa na mtandao mkubwa ndani ya chama kupata nafasi ya kuonekana CC. Hili linaongeza ushindani wa haki, ubunifu na kupanua hazina ya uongozi.

Kuimarisha demokrasia ya ndani ya Chama

Kwa mujibu wa Utafiti wa Twaweza wa mwaka 2023, asilimia 64 ya Watanzania walieleza kuwa vyama vya siasa havina demokrasia ya kweli ndani ya mfumo wao. Kwa CCM kufanya mabadiliko haya, inakuwa mfano kwa vyama vingine kwa kuonyesha namna demokrasia inaweza kuishi ndani ya taasisi kubwa ya kisiasa.

Marekebisho ya Ibara ya 99(3)(f) si tu mabadiliko ya vifungu vya Katiba, ni mageuzi ya fikra, mwelekeo na dhamira ya dhati ya kukijenga chama chenye kupambana na changamoto za sasa kwa uhalisia.

Katika hili, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameandika historia nyingine ya uongozi wa kisasa unaotanguliza maamuzi ya pamoja, usawa, na ufanisi.

Kwa msingi huu, wanachama wa CCM na Watanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kuona kwamba chama chao kiko katika mikono salama, chini ya nahodha aliye tayari kusikia na kuchukua hatua. Hakika, huu ni ushindi wa mageuzi ya kweli.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *