Uongozi wa Fountain Gate unadaiwa kumsimamisha kipa wake Mnigeria, John Noble kwa makosa yanayodaiwa kuwa ni ya kizembe mna kuigharimu timu hiyo kukubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Yanga.

Noble amefungwa mabao mawili kati ya manne waliyofungwa na Yanga akicheza kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza kabla ya benchi la ufundi kufanya uamuzi wa kufanya mabadiliko kumwingiza kipa mwingine ambaye naye alifungwa mabao mawili.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo kimeliambia Mwananchi kuwa ni kweli wamefanya uamuzi wa kumsimamisha mchezaji huyo kutokana na kufanya makosa mawili yaliyoigharimu timu hiyo.
“Ni kweli tumemsimamisha hatujapendezwa na makosa aliyoyafanya ambayo yamesababisha timu yetu kuondolewa mchezoni kutokana na uzembe wa mtu mmoja ambaye ameighalimu timu nzima,” kimesema chanzo hicho.
Kocha wa Fountain Gate, Robert Matano baada ya mchezo wa jana dhidi ya Yanga alisema; “Golikipa leo amewapa mabao. Ametuangusha kabisa golikipa wa aina yake kufanya makosa kama yale, sasa kama tunacheza vizuri halafu tunapeana mabao vile itakuwa vigumu sisi kushinda,” alisema na kuongeza;
“Hawezi kufanya makosa kama yale golikipa wa kariba ya juu kama yeye ametutoa mchezoni kabisa, kwa mabao aliyofungwa hakuna timu yoyote hata Yanga pia wangeanza kufungwa mabao kama yale wangetoka mchezoni.”
Fountain Gate imefungwa na Yanga jumla ya mabao 9-0 katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufungwa 5-0 katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza Desemba 29, 2024.