Kocha wa zamani wa Kagera Sugar na Dodoma Jiji, Francis Baraza, yuko kwenye hatua za mwisho kukamilisha makubaliano ya kuifundisha Pamba Jiji katika msimu ujao wa Ligi Kuu.

Baraza amesema mazungumzo kati yake na uongozi wa klabu hiyo yamekamilika kwa asilimia 80 na kinachosubiriwa ni kusaini mkataba na kutangazwa rasmi. Atachukua nafasi ya Fred Felix Minziro ambaye huenda akashushwa kuwa msaidizi au kuondoka kabisa.
Uongozi wa Pamba Jiji umevutiwa na rekodi ya Baraza alipokuwa na Kagera Sugar, na unaamini atasaidia kuboresha matokeo msimu ujao.
“Tumefikia pazuri kwenye mazungumzo. Nimevutiwa na mipango yao na namna menejimenti ilivyo tayari kusaidia benchi la ufundi. Tunachotakiwa ni kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Baraza.
Pamba Jiji ilimaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya 11 kwa alama 34, na ilinusurika kucheza mchujo kwa tofauti ndogo ya alama.