IMF yafikia makubaliano ya awali na Tanzania, dola milioni 441 kusaidia uchumi

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limetangaza kuwa limefikia makubaliano ya awali na Serikali ya Tanzania, ambayo yakipitishwa rasmi na bodi ya IMF, yataiwezesha nchi hiyo kupata takriban dola milioni 441 kwa ajili ya kuimarisha uchumi wake.

Fedha hizo ni sehemu ya mapitio ya tano ya Mpango wa Mikopo ya Muda Mrefu kupitia Dirisha la ECF (Extended Credit Facility) pamoja na mapitio ya pili ya Mpango wa Uhimilivu na Ustahimilivu (Resilience and Sustainability Facility – RSF).

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya ujumbe wa IMF, ukiongozwa na Nicolas Blancher, kufanya ziara rasmi nchini Tanzania kati ya Aprili 2 hadi 17, 2025. Wakati wa ziara hiyo, ujumbe huo ulifanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa serikali akiwemo Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo.

Katika taarifa yao, IMF imeeleza kuwa kwa ujumla hali ya uchumi wa Tanzania ni imara, huku pato la taifa (GDP) likikua kwa asilimia 5.5 mwaka 2024, na linatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 6 mwaka 2025.

Aidha, mfumuko wa bei umeendelea kudhibitiwa na kufikia asilimia 3.3 kufikia Machi 2025, chini ya lengo la asilimia 5 lililowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Hata hivyo, IMF imeonya kuhusu uwepo wa changamoto kadhaa zinazoweza kuathiri mwenendo wa uchumi wa nchi, zikiwemo hali ya sintofahamu katika mazingira ya kiuchumi kimataifa, migogoro katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na uchaguzi mkuu ujao nchini Tanzania ambao unaweza kuongeza matumizi ya serikali au kusababisha ucheleweshwaji wa utekelezaji wa mageuzi ya kiuchumi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *