Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu Tanzania (TAFF) limemtangaza Ivo Mapunda kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu ya Taifa ya Tembo Warriors kwa mkataba wa mwaka mmoja. Mapunda alikuwa kocha wa magolikipa wa timu hiyo kwenye Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Uturuki.

TAFF imesema Mapunda ataanza kazi rasmi wiki ijayo kwa maandalizi ya michuano ya CECAAF ya Afrika Mashariki na Kati itakayofanyika Septemba nchini Burundi.
Wakati huo huo, TAFF imekabidhi zawadi kwa timu zilizofanya vizuri kwenye mashindano ya hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Ubungo FC ilishinda Sh. 1,000,000, Sauti Parasports Sh. 500,000 na Arusha Warriors Sh. 250,000. Timu zote zilishiriki pia zilipewa Sh. 400,000 kwa kila moja pamoja na huduma za malazi, chakula na usafiri.