Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametangaza kuwa amri mpya imetolewa kwa wanajeshi wa nchi hiyo kumkamata mwanasiasa wa upinzani, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, akiwa hai au amekufa.
Akizungumza kupitia mtandao wa kijamii wa X, Jenerali Muhoozi amesema walisitisha kwa muda wa saa 24 operesheni za kumtafuta Bobi Wine kwa maelekezo ya Kamanda Mkuu wa Majeshi, Rais Yoweri Museveni, aliyeshinda tena uchaguzi wa hivi karibuni na kuchaguliwa kwa muhula wa saba kuiongoza Uganda.
Kwa mujibu wa Muhoozi, hatua hiyo ililenga kumpa Bobi Wine fursa ya kujisalimisha kwa amani, hata hivyo hakufanya hivyo ndani ya muda uliotolewa, hali iliyopelekea operesheni za kijeshi kuendelea.
Bobi Wine amekuwa mafichoni tangu kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, akidai kuwepo kwa njama ya kutaka kumdhuru. Wiki iliyopita, Muhoozi alimpa Bobi Wine saa 48 kujisalimisha kwa Polisi, lakini alishindwa kufanya hivyo, huku jitihada za kumtafuta zikiendelea bila mafanikio.
Inaelezwa kuwa Bobi Wine alitoroka nyumbani kwake Ijumaa, tarehe 16 ya mwezi huu, baada ya wanajeshi kufika eneo hilo siku moja kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Katika uchaguzi huo, Rais Yoweri Museveni alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 71 ya kura, huku mpinzani wake Bobi Wine akipata asilimia 24.
Akizungumza kuhusu sakata hilo, Jenerali Muhoozi alinukuliwa akisema:
“Tulisitisha utafutaji wetu wa Kabobi kwa saa 24 kwa maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu. Inaonekana, kulingana na baadhi ya vyanzo, alitaka kujisalimisha kwa amani. Hajajisalimisha popote. Sasa askari wetu wamepewa amri ya kumkamata akiwa hai au akiwa amekufa.”
Aidha, alikanusha madai ya askari kumpiga mke wa Bobi Wine akisema:
“Askari wangu hawakumpiga Barbie, mke wa Kabobi. Kwanza kabisa, hatuwapigi wanawake. Tunamtafuta mume wake, si yeye.”




