Klabu ya JKT Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kufanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiahidi kuepuka hali iliyoikumba msimu uliopita, ambapo ilihitaji mechi za mchujo (play off) ili kusalia ligi kuu.

Meneja wa timu hiyo, Ashraf Omari, amesema msimu huu wanataka kujihakikishia nafasi salama mapema kwa kushinda michezo muhimu badala ya kusubiri matokeo ya mwisho.
“Tunalenga kusalia Ligi Kuu bila presha ya play off au kuanza kufanya mahesabu ya vidole mwishoni. Ndiyo maana tunataka kushinda mechi zitakazotuweka katika eneo salama mapema,” alisema Omari.
JKT Tanzania inajiandaa kwa mchezo wake wa raundi ya 17 dhidi ya Coastal Union, utakaopigwa Ijumaa ijayo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Msimu uliopita, JKT Tanzania ilinusurika kushuka daraja baada ya kuifunga Tabora United mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku mchezo wa marudiano ukimalizika kwa sare. Tabora United nayo iliokoka kwa kushinda play off ya pili dhidi ya Biashara United kwa jumla ya mabao 2-1.
Kwa sasa, JKT Tanzania inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 19 baada ya michezo 16. Imeshinda mechi nne, sare saba na kupoteza tano, huku ikifunga mabao 10 na kuruhusu 12.