Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa usimamizi mzuri wa vitega uchumi vyake, ambavyo kwa sasa vinajiendesha kwa faida.

Kauli hiyo imetolewa Machi 12, 2025, jijini Arusha na wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Fatma Taufiq, wakati wa ziara yao katika mradi wa makazi wa Olorien.
“Kwa kweli nawapongeza PSSSF kwa kusimamia vyema mradi huu, ambao tumeelezwa kuwa umeshaanza kuingiza faida. Hongereni sana. Hata hivyo, pongezi za dhati ziende kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutoa miongozo bora iliyowezesha PSSSF kuendesha vyema miradi hii,” alisema Mhe. Taufiq.
Mafanikio ya PSSSF katika malipo ya mafao
Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa PSSSF imeimarisha ulipaji wa mafao kwa wanachama wake, tofauti na ilivyokuwa awali.
“Hivi sasa hakuna malalamiko mengi kuhusu ucheleweshaji wa mafao. Nawapongeza kwa utunzaji mzuri wa fedha za wanachama kwa kuwekeza katika miradi yenye tija. Endeleeni na mwenendo huu mzuri,” aliongeza.



Serikali yaahidi kuendelea kusimamia mfuko
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete, alisema serikali imepokea maelekezo na ushauri wa kamati na itaendelea kuyafanyia kazi ili kuongeza tija katika uwekezaji wa mfuko huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul-Razaq Badru, alisema hali ya uhimilivu wa mfuko huo ni nzuri, thamani yake inazidi kuongezeka, na wanachama wake wanalipwa kwa wakati na kwa usahihi.
Kamati yaendelea na ziara ya kukagua miradi ya umma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii inaendelea na ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali ya taasisi za umma ili kujionea uendeshaji wake na kutoa maelekezo ya kuboresha zaidi uwekezaji wa serikali.

