Dar es Salaam
Katika msimu mpya wa mashindano maarufu ya soka kwa vijana wa mitaani, Ndondo Cup, kampuni ya mawasiliano ya YAS imetangaza rasmi kuwa mdhamini mkuu wa toleo la mwaka 2025 — hatua iliyopokelewa kwa hamasa kubwa na wadau wa michezo kote nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa udhamini huo, Robert Kasulwa, Mkurugenzi wa YAS Kanda ya Dar es Salaam Kusini, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kampeni ya kampuni hiyo ijulikanayo kama “Anzia Ulipo”, inayolenga kuwahamasisha vijana kutafuta mafanikio kuanzia walipo — mitaani, vijijini, au maeneo ya pembezoni.
“Tunawaamini vijana hawa. Tunaamini kuwa kupitia teknolojia yetu ya kisasa kama vile huduma za intaneti za kasi ya 4G na 5G, tunaweza kuwapa nguvu ya kufikia ndoto zao. Ndondo Cup ni jukwaa halisi la vipaji halisi,” alisema Kasulwa.
Mashindano ya Ndondo Cup mwaka huu yameingia hatua ya mtoano zikiwa zimebakia timu 32. Ushindani umekuwa wa hali ya juu huku kila timu ikisaka nafasi ya kutinga hatua ya mwisho. Kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo, mshindi wa kwanza atazawadiwa kitita cha shilingi milioni 30 — ongezeko kubwa ikilinganishwa na zawadi za misimu ya nyuma.
Waandaaji wa mashindano wamesema kuwa udhamini wa YAS haumaanishi tu ongezeko la thamani ya kifedha, bali pia unatoa motisha na matumaini kwa vijana wengi waliokuwa hawana majukwaa ya kuonyesha vipaji vyao. Kupitia mashindano haya, wachezaji wengi wamepata fursa za kitaifa na hata kimataifa, na sasa matarajio yamezidi kuongezeka.


