Kiliba kuongoza wanavyuo Dodoma kuweka maazimio ya wasomi kuhusu Uchaguzi Mkuu 2025

Kampeni ya Mama Asemewe chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Kiliba, imeandaa kongamano kubwa la wanavyuo kutoka Vyuo mbalimbali mkoani Dodoma, litakalofanyika tarehe 29 Machi 2025 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre.

Kongamano hilo linalenga kuwakutanisha wasomi kwa ajili ya kujadili na kuweka maazimio ya pamoja kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, likiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato huo wa kidemokrasia kwa msingi wa uelewa na uzalendo kwa taifa.

Kiliba, kama kiongozi wa kampeni ya Mama Asemewe ataongoza mchakato wa maazimio hayo, ambapo wanavyuo watatoa mtazamo wao kuhusu mustakabali wa Tanzania na namna vijana wanavyoweza kushiriki katika kujenga taifa imara kupitia uchaguzi huu muhimu wa mwaka 2025.

Akizungumza juu ya kongamano hilo, Kiliba amesema: “Wasomi wana nafasi kubwa katika kuleta maendeleo ya taifa letu.

Hili si tu kongamano la mijadala, bali ni jukwaa la kuweka maazimio yatakayoonyesha msimamo wa wanavyuo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Tunataka vijana waonyeshe uzalendo, wawe sehemu ya maamuzi, na wahakikishe kwamba maendeleo yanakuwa ajenda kuu katika uchaguzi wa 2025

“Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa vyuo vikuu, wanazuoni, pamoja na wadau wa maendeleo na demokrasia nchini, huku likipewa kipaumbele maalum kama sehemu ya harakati za kuhakikisha sauti ya vijana wasomi inasikika katika ujenzi wa taifa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *