Kipa Kagera Sugar ataja kinachowatafuna

GOLIKIPA wa Kagera Sugar, Ramadhani Chalamanda, amesema timu yao imekuwa ikifanya vibaya kwenye mechi za Ligi Kuu kutokana na makosa binafsi ya wachezaji na si kitu kingine.

Kipa huyo namba moja wa timu hiyo, aliyasema hayo siku moja tu baada ya mchezo wa Ligi Kuu kati ya timu yake na Yanga, uliochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, ambapo alikaa langoni na kulambishwa mabao 4-0.

Alisema si mechi dhidi ya Yanga tu, bali michezo mingi wamekuwa wakifungwa kutokana na makosa binafsi na si ya kimfumo, hivyo anadhani walimu wake wataendelea kulifanyia kazi suala hilo.

“Mechi nyingi tunapoteza kutokana na makosa binafsi, makosa ya mchezaji mmoja mmoja, ndiyo yaliyotufikisha hapa, ukiangalia kwenye mchezo wetu dhidi ya Yanga ni vile, tumefungwa kwa makosa yetu wenyewe, kila bao lilitokana na makosa tunayoyafanya.

Kwenye mpira wa miguu makosa huwa hayakosekani, ndiyo maana kila siku kuna mazoezi na si kila mkifanya mtayamaliza, ila mtayapunguza tu, mnaweza kupunguza kosa hili likazaa lingine jipya, lakini inabidi tuyapunguze sana kwenye timu yetu,” alisema kipa huyo ambaye alifanya kazi kubwa sana ya kuokoa hatari zilizoonekana kuzaa mabao, huku pia akipangua mkwaju wa penalti wa Stephane Aziz Ki.

Kagera Sugar iko nafasi ya 15 ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 11 tu, kwa michezo 16 iliyocheza, ikishinda miwili tu, sare tano na kupoteza tisa.

Akizungumzia kiwango chake bora, Chalamanda ambaye alichaguliwa kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars kilichocheza michuano ya Kombe la Mapinduzi mwezi uliopita, Zanzibar, alisema anajaribu kuzikimbilia ndoto zake za kufika mbali kwenye mchezo huo.

“Najaribu kuzikimbilia ndoto zangu, siyo kuishia hapa Kagera Sugar, nataka kufika mbali zaidi kwenda timu kubwa zaidi ya hapa, kwa sababu hii ndiyo kazi yangu niliyoichagua, shule sina, kwa hiyo nitafanya vizuri ili nipate riziki,” alisema kipa huyo.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *