Na Mwandishi Wetu
Kocha wa Taifa Stars, Hemed Morocco, amesema mashindano ya CECAFA 4 Nations hayajaja kwa wakati muafaka, kwa kuwa yanaingiliana na maandalizi ya timu hiyo kuelekea Fainali za CHAN zitakazoanza Agosti 2.

Morocco ameeleza hofu kuwa wachezaji wake watakuwa na uchovu kwa kucheza mechi tatu za CECAFA ndani ya siku tano, kabla ya kukutana na Burkina Faso katika mechi ya ufunguzi ya CHAN.
“Michuano hii ni mizuri, lakini imetubana sana. Kama ingekuja wiki mbili zilizopita ingesaidia zaidi. Tunapaswa kucheza mechi tatu mfululizo halafu baada ya hapo tuingie CHAN. Itakuwa changamoto,” alisema Morocco.
Stars itaanza kampeni ya CECAFA kwa kuvaana na Congo Brazaville Julai 22, kisha Kenya Julai 24, na kumalizia na Uganda Julai 27, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite, Babati.
Morocco amesema, licha ya changamoto hizo, wachezaji wake wako kwenye hali nzuri ya kimwili na kiakili baada ya kambi nzuri mjini Ismailia, Misri.
Stars ipo Kundi B katika CHAN pamoja na Burkina Faso, Afrika ya Kati, Madagascar na Mauritania.