Kusaga ampa mwaliko maalum Rais Samia Tuzo za Malkia wa Nguvu Dar

Clouds Media Group imezindua rasmi msimu mpya wa Malkia wa Nguvu 2025 kwa kauli mbiu ya “TWENDE DUNIANI”, ikitangaza kuwa mwaka huu mashindano hayo yatafanyika katika kanda tano za Tanzania.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga, alisema kuwa ndoto yake ya muda mrefu ilikuwa ni kuanzisha jukwaa maalum kwa wanawake, ambalo sasa limefanikiwa licha ya changamoto za awali.

“Azma na maono yangu kwa miaka 30 iliyopita ni kuwa na jukwaa ambalo wanawake watahusika kwenye kila kitu ninachokifanya. Wazo la tuzo hizi lilianzia kwa mwanamke mjasiriamali aitwaye Mwanamakuka, na tuliona ni vyema kulifanya kuwa kubwa zaidi. Ndicho tunachosherehekea leo,” alisema Kusaga.

UZINDUZI WA REDIO MPYA YA WANAWAKE – MALKIA CHOICE FM

Katika hatua nyingine, Clouds Media Group imetangaza kuanzisha redio mpya maalum kwa wanawake inayoitwa Malkia Choice FM. Kusaga alisema redio hiyo itakuwa sauti ya wanawake, ikilenga kuwawezesha na kuwahamasisha katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

“Sisi tunaamini wanawake ni bora sana duniani. Siku ya tarehe 04 Aprili 2025 tunamualika Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, najua anatusikiliza watoto wake, ili tusherehekee naye siku kubwa ya Malkia wa Nguvu jijini Dar es Salaam,” aliongeza Kusaga.

MALKIA WA NGUVU 2025 KUPITA KATIKA KANDA TANO

Kwa mwaka huu, Tuzo za Malkia wa Nguvu 2025 zitafanyika katika kanda tano za Tanzania, ambazo ni:

Kanda ya Ziwa
Kanda ya Kati
Nyanda za Juu Kusini
Kanda ya Kaskazini
Kanda ya Pwani

Kwa mara nyingine, Clouds Media Group imeonyesha dhamira yake ya kuendelea kuinua na kuthamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *