Bandari Kavu ya Kwala, iliyoko Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, sasa imekuwa mkombozi wa msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kulingana na taarifa rasmi, Bandari ya Kwala ina uwezo wa kushughulikia zaidi ya makasha 823 kwa siku, sawa na takribani 300,000 kwa mwaka.
Hii ina maana kuwa mamilioni ya bidhaa sasa zinapitishwa kwa haraka zaidi, gharama ndogo na kwa usalama mkubwa.
Bandari hiyo imeunganishwa moja kwa moja na reli ya kisasa ya SGR, ikimaanisha mzigo unateremka bandarini Dar es Salaam, unapakiwa moja kwa moja kwenye treni na kufika Kwala kwa muda mfupi.
Huu ndio mfumo wa kisasa wa multimodal transport ambao Tanzania ilikuwa ikiuhitaji kwa muda mrefu.

Kwala ni viwanda, ajira na biashara
Lakini Rais Dkt. Samia hakusimama kwenye mizigo tu. Kupitia Kwala Industrial Park, eneo hili linabadilishwa kuwa kituo kikuu cha viwanda barani Afrika.
Zaidi ya hekta 1,000 zimetengwa kwa ajili ya viwanda zaidi ya 200, vyenye thamani ya dola bilioni 3, huku vikiwa na uwezo wa kuzalisha ajira zaidi ya 300,000, zikiwemo 50,000 za moja kwa moja.
Hili ni jibu la Taifa kwa changamoto ya ajira kwa vijana. Kila kiwanda kinachojengwa ni nafasi ya kijana mmoja kujikomboa kiuchumi. Kila kontena linaloshushwa Kwala lina maana ya mkulima anayepata soko, mfanyabiashara anayepata faida na familia inayopata matumaini mapya.

Kwala ni Tanzania mpya inayoaminika
Wakati Tanzania inapambana kujitangaza kama kitovu cha biashara Afrika Mashariki, Kwala imekuwa nyenzo muhimu ya kufanikisha hilo.
Imeanza kuhudumia si tu Tanzania, bali pia nchi kama Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda na Uganda ambazo sasa zinaona faida ya kupitisha mizigo kupitia Tanzania kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi.
Huu ni ushahidi kuwa maono ya Rais Dkt. Samia si ya ndani tu, bali ni ya kikanda. Yanaipa Tanzania nafasi ya kuwa Taifa kiongozi katika biashara ya Afrika Mashariki na kati.
Kumwandika Dkt. Samia ni kumwandika kiongozi mwenye mwelekeo. Sio wa maneno matupu, bali wa vitendo vyenye mashiko. Mradi wa Bandari ya Kwala ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda yake ya Tanzania yenye uchumi wa viwanda, usafirishaji wa kisasa, na biashara jumuishi.
Rais Dkt. Samia amekuwa mstari wa mbele kuvutia wawekezaji, kuondoa vikwazo vya urasimu na kuhakikisha miradi kama Kwala inakamilika kwa wakati.
Leo hii, Kwala ni kielelezo cha Tanzania mpya. Ni sehemu ya ndoto kubwa ya kuwa taifa lenye viwanda, lenye ajira, lenye mifumo ya kisasa ya usafiri, na lenye kiongozi anayeona mbali zaidi ya mwaka huu au ujao.
Katika Kwala, tunaona dira ya Dkt. Samia ikiishi. Tunaona siasa zikiwa siyo tena za maneno bali za maendeleo yanayogusa umma. Tunaona Tanzania inayoshindana duniani.

