Lukuvi aagiza uboreshaji wa mawasiliano ya tahadhari za maafa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, ameielekeza Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kujiratibu vyema katika kusambaza taarifa za tahadhari ya maafa kwa wakati, ili hatua za mapema zichukuliwe kabla ya madhara kutokea.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, ameielekeza Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kujiratibu vyema katika kusambaza taarifa za tahadhari ya maafa kwa wakati, ili hatua za mapema zichukuliwe kabla ya madhara kutokea.

Lukuvi alitoa maagizo hayo jana, Februari 26, 2025, alipotembelea Kituo cha Ufuatiliaji wa Majanga kilichopo ndani ya Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

“Kwa nafasi mliyonayo na teknolojia mnazotumia, mnaweza kupata na kusambaza taarifa za tahadhari bila urasimu. Ni muhimu kuhakikisha taarifa hizi zinawafikia wahusika kwa haraka ili kuepusha athari kubwa za maafa,” alisisitiza Waziri Lukuvi.

Ameelekeza pia kuwe na njia rahisi za mawasiliano, ikiwemo upatikanaji wa taarifa za tahadhari kupitia simu kila siku, ili wananchi waweze kupata taarifa hizo kwa urahisi na kuchukua tahadhari stahiki.

“Huduma hii iwe bure na ipatikane muda wote. Wananchi waingie, wasome, na wachukue tahadhari mapema. Hii itahakikisha tunatimiza wajibu wetu ipasavyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura katika Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jane Kikunya, alieleza kuwa kituo hicho kina jukumu kubwa la kufuatilia majanga na kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutoa taarifa za awali za tahadhari kwa ngazi tofauti.

Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Maafa ya mwaka 2022, kila Mkoa unatakiwa kuwa na kituo cha usimamizi wa maafa ili kurahisisha ufuatiliaji wa majanga katika maeneo husika.

Ofisi ya Waziri Mkuu inafuatilia uanzishwaji wa vituo hivyo kwa kushirikiana na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa, ambao kisheria wamepewa jukumu la kusimamia vituo hivyo. Hatua hii inalenga kujenga uelewa wa miongozo ya uanzishaji na usimamizi wa vituo vya maafa nchini.

“Vituo vya Mikoa vitaunganishwa na mifumo ya Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura ili kurahisisha ufuatiliaji wa majanga kwa ukaribu zaidi,” alibainisha Jane.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *