Madereva 477 wafaulu usaili wa ajira Qatar – 28 wawasili awamu ya kwanza

Zoezi la usaili kwa madereva 800 wa Kitanzania wanaotarajiwa kwenda kufanya kazi nchini Qatar limeanza rasmi katika Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Katika awamu ya kwanza ya usaili, jumla ya madereva 477 kati ya 800 waliotarajiwa wamefaulu na kupangiwa nafasi za kazi nchini Qatar kupitia Kampuni ya Usafirishaji ya Mowasalat (Karwa).

Julai 28, 2028, madereva 28 kati ya 103 waliopangwa kuondoka katika awamu ya kwanza wamewasili salama nchini Qatar. Madereva wengine wanatarajiwa kuwasili kati ya jana Julai 29 na leo Julai 30 na Agosti 1-3, 2028, ili kukamilisha idadi ya madereva 103 kwa awamu hiyo ya kwanza. Waliobaki watawasili kwa awamu zinazofuata mara tu taratibu za visa na tiketi zitakapokamilika.

Usaili huo ni sehemu ya mpango maalum wa kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata ajira katika sekta ya usafirishaji nchini Qatar. Zoezi hili linatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Kampuni ya Mowasalat (Karwa), Mawakala wa Ajira kutoka Tanzania na Qatar, na Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar, chini ya uongozi wa Balozi Habibu Awesi Mohamed.

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya Mowasalat imepanga pia kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) katika maeneo ya mafunzo ya udereva, ufundi na usafirishaji. Makubaliano haya yatahusisha Chuo cha Mafunzo cha Karwa (Qatar), NIT, VETA na Chuo cha Karume – Zanzibar.

Usaili umegawanywa katika makundi manne kwa uratibu wa wakala mbalimbali wa ajira. Awamu ya kwanza inayoratibiwa na Kampuni ya Sassy Solutions (Tanzania) na Waha (Qatar), ilianza tarehe 27 Mei. Wakala wengine ni pamoja na Mkapa Foundation, Larali na Connect.

Vipengele vya usaili vinajumuisha mtihani wa nadharia na mtihani wa vitendo, ambapo waombaji huendesha magari barabarani ili kuonesha ujuzi wao wa udereva.

Mwitikio wa vijana umeelezwa kuwa mkubwa, huku wengi wakijitokeza kwa matumaini ya kupata ajira nje ya nchi. Serikali imesisitiza kuwa inafuatilia kwa karibu mchakato mzima kuhakikisha uwazi, haki na usalama kwa washiriki wote.

Zoezi hili linatarajiwa kuongeza ajira kwa mamia ya Watanzania na kukuza uhusiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Qatar.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *