Diwani Mteule wa Kata ya Tumbi, Manispaa ya Kibaha, Dk. Mawazo Nicas, ni miongoni mwa madiwani wanne waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya Meya wa Manispaa ya Kibaha kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini.
Wengine waliouchukua fomu ni Mashaka Mahande kutoka Sofu, John Katele wa Pangani, pamoja na Elinius Mapunda.
Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 21 ofisini kwake, Kaimu Katibu wa CCM Kibaha Mjini, Latifa Semwanza, alisema zoezi la utoaji wa fomu lilianza Novemba 20 na limehitimishwa leo saa 10 jioni.
Semwanza, ambaye pia ni Kiongozi ndani ya Jumuiya ya Wazazi, aliwataja waliochukua fomu za kuwania nafasi ya Naibu Meya kuwa ni Ally Simba wa Misugusugu, Aziza Mruma (Viti Maalum) na Ramadhani Lutambi wa Mailimoja.
Kaimu katibu huyo alibainisha kuwa baada ya kukamilika kwa hatua ya kuchukua na kurejesha fomu, kinachofuata sasa ni vikao vya ndani ya chama kwa ajili ya kufanya mchujo na uteuzi wa wagombea.





