Benki ya NMB imeanzisha huduma ya utoaji bima kwa mazao na mifugo nchini kama sehemu ya mkakati wake wa kusaidia ukuaji wa sekta ya kilimo na ufugaji, ambapo hadi sasa mifugo zaidi ya 2,000 tayari imekatiwa bima.

Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Bi. Janeth Shongo, alitoa taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea banda la benki hiyo katika viwanja vya maonesho ya wakulima ya Nane Nane, yanayofanyika jijini Dodoma.
Bi. Shongo alisema hadi sasa ng’ombe wapatao 2,000 wamekatiwa bima na wafugaji mbalimbali, ambapo gharama ya chini ya bima hiyo ni Shilingi 20,000 kwa mnyama mmoja, huku thamani ya jumla ya bima hizo ikikadiriwa kufikia Shilingi bilioni 1.5.
“Tumeleta mapinduzi makubwa katika sekta hii ili kuhakikisha mfugaji hana wasiwasi na shughuli zake. Kwa mfano, iwapo atapata majanga kama kifo cha mifugo, basi atakuwa na uhakika wa fidia kupitia bima aliyokata,” alisema Shongo.
Kwa upande wa kilimo, Shongo alibainisha kuwa zaidi ya wakulima 300,000 wamefikiwa na huduma ya bima ya mazao, ambapo thamani ya bima iliyotolewa katika sekta hiyo imefikia takribani Shilingi bilioni 658.
Aidha, alitoa wito kwa wakulima kote nchini kuchangamkia fursa hiyo kwa ajili ya kulinda mazao yao dhidi ya majanga kama vile ukame, mafuriko na magonjwa.
Katika hatua nyingine, Bi. Shongo alisema NMB imeweza kukopesha zaidi ya Shilingi bilioni 100 kwa wafugaji nchini, ikiwa ni mikopo yenye masharti nafuu na riba rafiki, inayolenga kumwezesha mfugaji, mkulima na mvuvi kuinua maisha yao kupitia shughuli zao.




“Tunatoa mikopo rahisi inayolenga watu wa kipato cha chini. Tunawakaribisha wananchi wote walioko katika sekta hizi watufikie ili wanufaike na fursa hii,” aliongeza.
Shongo alibainisha pia kuwa benki hiyo imejikita katika kutoa elimu ya kifedha na ujasiriamali kupitia vyama vya ushirika vya wakulima (AMCOS), ambapo hadi sasa NMB imefikia AMCOS 1,139 na viongozi wa wakulima zaidi ya 38,000, kati yao wanawake ni 12,000.
“Elimu tunayotoa inajumuisha uongozi bora wa vyama, matumizi ya huduma za kifedha, na mbinu bora za kilimo na ufugaji. Viongozi hawa wa AMCOS watawafundisha wakulima wenzao ili kuongeza tija katika uzalishaji,” alisema.
Benki hiyo pia imetoa elimu ya kifedha kwa zaidi ya vijiji 2,000, ikiwafikia wananchi zaidi ya milioni 2.4 walioweza kufungua akaunti, kupata elimu ya matumizi ya NMB Mkononi na huduma za mawakala wa NMB (NMB Wakala).
Katika maonesho ya mwaka huu ya Nane Nane, NMB imeahidi kuendelea kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, pamoja na kupanua wigo wa huduma zake hadi vijijini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
