Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi, ametamba kuwa anaiandaa timu yake kupata ushindi mkubwa dhidi ya Dodoma Jiji FC, kama ilivyofanya dhidi ya Tanzania Prisons (5-0), ili kujiweka sawa kuelekea dabi na Simba.

Yanga itacheza dhidi ya Dodoma Jiji Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Hamdi amesema ushindi huo ni muhimu kwa sababu “baada ya Jumapili tuna mchezo wa maamuzi ya ubingwa dhidi ya Simba.”
Alikataa kufichua mbinu atakazotumia lakini alisisitiza kuwa wana kila sababu ya kupambana ili kuendeleza ushindi.
Katika mechi dhidi ya Prisons, mabao ya Yanga yalifungwa na Pacome Zouzoua (2), Mudathir Yahya, Clatous Chama na Israel Mwenda. Ushindi huo umeiweka Yanga kileleni na pointi 76, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 75.
Kocha wa Prisons, Amani Josiah, alisema timu yake ilikosa nidhamu ya mchezo, kufanya makosa binafsi na kukumbana na ubora wa Yanga, akieleza kuwa sasa wanapambana kuepuka kushuka daraja.