Dar es Salaam. Kampuni ya Honora Tanzania kupitia huduma yake ya Mixx by Yas imetia saini makubaliano ya kimkakati na Kampuni ya EACLC pamoja na Honora Tanzania Mobile Solutions Limited, katika hafla maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Makubaliano hayo yanaashiria hatua kubwa katika maendeleo ya biashara, teknolojia ya kifedha na huduma za kijamii kwa Watanzania, hususan katika kuimarisha biashara na huduma za e-commerce kupitia mifumo ya kidigitali.
Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa Mixx by Yas alisema, “Makubaliano haya siyo tu ya kiutaratibu, bali yanaonesha dhamira yetu ya pamoja ya kujenga mazingira bora ya biashara yanayoendeshwa kidigitali, kwa haraka na kwa urahisi zaidi kwa kutumia teknolojia za kifedha.”
Kupitia ushirikiano huo, huduma mbalimbali za kifedha zitapatikana kwa urahisi kwa wafanyabiashara waliopo ndani ya mradi mkubwa wa biashara wa EACLC unaojengwa eneo la Ubungo, Dar es Salaam. Mradi huo unatarajiwa kuwa na zaidi ya wafanyabiashara 2,000, na utakuwa kitovu cha kisasa cha biashara kilicho na mifumo kamili ya kidigitali.



Faida kwa Wafanyabiashara na Wananchi
Mkurugenzi huyo alifafanua baadhi ya manufaa ambayo wafanyabiashara na wananchi watapata kupitia ushirikiano huo:
- Malipo kwa Simu (Lipa kwa Simu): Wafanyabiashara wataweza kupokea malipo ya bidhaa na huduma moja kwa moja kwa njia ya simu, hivyo kuondoa matumizi ya fedha taslimu.
- Malipo ya Kodi ya Pango: Wapangaji wa maduka na ofisi katika mradi huo wataweza kulipa kodi zao kwa njia ya kidigitali bila kero ya foleni au makaratasi.
- Malipo kwa Wafanyakazi na Wazabuni: Makampuni yatakuwa na uwezo wa kuwalipa wafanyakazi mishahara, pamoja na malipo kwa wazabuni kwa njia ya kidigitali kwa usahihi na kwa wakati.
- Malipo kwa Biashara Mtandaoni: Biashara zitakazokuwa ndani ya EACLC zitakuwa na uwezo wa kuunganisha mfumo wa malipo ya moja kwa moja kwa wateja wao mtandaoni.
- Ripoti za Fedha kwa Wakati: Kila muamala utakuwa na ripoti ya moja kwa moja ya kidigitali, hivyo kuongeza uwazi na uwajibikaji wa kifedha.
- Huduma za Wakala: Eneo hilo litakuwa na mawakala na duka la Yas litakalosaidia huduma za kuweka na kutoa fedha kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Mixx by Yas, huduma hizo zitakwenda sambamba na mafunzo na msaada wa kitaalamu kwa wafanyakazi wa EACLC pamoja na wapangaji wote, kuhakikisha kila mmoja anatumia mifumo hiyo kwa ufanisi.
“Teknolojia ni nzuri, lakini tunajua uzoefu wa mtumiaji ndio msingi wa mafanikio ya mifumo ya kidigitali. Tutaendesha mafunzo ya kina na kutoa msaada wa kudumu kwa wafanyabiashara wote ili kuhakikisha wanafaidika ipasavyo,” alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wa usalama wa taarifa za wateja na miamala, kampuni hiyo imethibitisha kuwa inaendesha shughuli zake kwa kufuata sheria za Tanzania, ikizingatia kikamilifu kanuni za kulinda taarifa za wateja pamoja na taratibu za kudhibiti utakatishaji wa fedha.
“Ushirikiano huu ni hatua kubwa kwa Mixx by Yas na kwa Tanzania kwa ujumla. Tunapongeza EACLC kwa mawazo yake bunifu katika sekta ya maendeleo ya biashara, na pia tunatambua mchango mkubwa wa wenzetu Honora Tanzania katika kuhakikisha tunafanikisha malengo haya ya pamoja,” alisema.
Akihitimisha hotuba yake, Mkurugenzi wa Mixx by Yas aliwahakikishia wafanyabiashara na wadau wote kuwa huduma bora, salama na rafiki zitaendelea kupatikana ili kuwarahisishia shughuli zao za kila siku.
“Lengo letu ni moja — kuhakikisha Watanzania wanafanya miamala ya kifedha kwa usalama, haraka na ufanisi zaidi ili waweze kuelekeza nguvu zao katika kukuza biashara zao. Mixx by Yas — Ni Zaidi ya Pesa.”




