Winga wa KenGold FC, Bernard Morrison, amesema asingekubali kutoka uwanjani hata kama angekuwa na mguu mmoja baada ya kugomea kubadilishwa katika mechi dhidi ya Simba waliyochapwa 5-0.

Morrison, ambaye alisifika kwa vituko alipokuwa Simba na Yanga, alisema yeye ndiye aliyekuwa anaisumbua Simba kuliko wachezaji wengine wa KenGold: “Hata kama ningebaki na mguu mmoja bado nisingetoka, nani kawasumbua mabeki wa Simba kama si mimi?”
Kocha wa KenGold, Omari Kapilima, alipanga kumtoa kipindi cha pili, lakini Morrison alikataa kwa ishara ya kichwa na kidole, akishangiliwa na mashabiki.
Ilikuwa mechi ya kwanza kwa Morrison kucheza dakika zote 90 tangu asajiliwe dirisha dogo. Mchezo wake wa kwanza ulikuwa dhidi ya Coastal Union alipoingia kipindi cha pili.