Mradi wa Maji Safi wa WaterAid watatua changamoto za maji na usafi Hanang’

Wananchi wa wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara, wanatarajia kunufaika na mradi wa maji utakaowapatia huduma ya maji safi kwa asilimia 100, huku wakiondokana na magonjwa ambukizi yanayotokana na uchafu wa mazingira na vyanzo vya maji.

Mradi huu unatekelezwa na shirika la WaterAid la Uingereza kwa kushirikiana na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) mkoani Manyara.

Akizungumza katika mkutano wa ushirikishwaji wa wadau mjini Katesh, Mkuu wa Miradi wa WaterAid Tanzania, Beda Levira, alieleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu. Levira alisema kuwa mradi wa mfano wa Hanang’ utatatua changamoto za upatikanaji wa maji safi, vyoo bora, na usafi wa mazingira, na utanufaisha wakazi wa vijiji 96 kutoka kata 33 za wilaya ya Hanang’.

“Mradi huu utahakikisha kuwa wananchi wanapata maji safi kwa asilimia 100 na kuondokana na changamoto za magonjwa ambukizi yanayotokana na uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji,” alisema Levira.

Mhandisi wa maji kutoka Ruwasa, Barnabas Taligunga, alisema kuwa mradi huo utaongeza nguvu ya uboreshaji wa miundombinu ya kusambaza maji kutoka kwenye vyanzo hadi kwa watumiaji ili kudhibiti magonjwa yanayosambazwa kupitia maji. Alisisitiza kuwa mradi huu ni wa mfano na utasaidia wilaya nyingine nchini kujifunza utekelezaji wake.

Kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, mganga mkuu wa mkoa, Dk. Andrew Method, alitoa wito kwa viongozi wa Hanang’ kutoa ushirikiano wa kutosha ili mradi huu uweze kufanikiwa na kuwa mfano kwa wilaya nyingine. Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kutekeleza mradi huu mkoani Manyara, hususan wilayani Hanang’, akisema kuwa utasaidia kutatua changamoto za afya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Programu za Kimataifa (IPD), WaterAid UK, Amaka Godfrey, alisema kuwa wataendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha mradi huu unawanufaisha wananchi wengi zaidi kwa kupata maji safi na salama. Aliongeza kuwa mbinu iliyotumika kufikia wilaya nzima ya Hanang’ ni nzuri na imekuwa na mafanikio katika nchi nyingine.

Wakazi wa wilaya ya Hanang’ wamesema wataulinda mradi huo ili uweze kuwanufaisha wao na vizazi vijavyo. Isack Mayomba, mmoja wa wakazi wa wilaya hiyo, alisema wanashukuru viongozi waliowezesha utekelezaji wa mradi huu. “Mwaka 2023 tulipatwa na matatizo makubwa, lakini leo 2025 tunapata mradi huu wa maji, ni jambo la kumshukuru Mungu,” alisema Mayomba.

Mradi huu unatarajiwa kuwa mfano mzuri kwa wilaya nyingine nchini katika kujifunza namna ya kutekeleza miradi ya maji safi na usafi wa mazingira.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *