📌 Asema mradi umefikia asilimia 99.8
📌 Awaasa watanzania kujivunia mradi wa Julius Nyerere
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ameipongeza Wizara ya Nishati kwa usimamizi bora wa mradi wa kimkakati wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere (JNHPP), ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115 na hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.

Msigwa alitoa pongezi hizo leo, Februari 16, 2025, alipokuwa katika eneo la mradi wa Julius Nyerere wakati wa Mkutano wa Msemaji Mkuu wa Serikali na waandishi wa habari. Mkutano huo ulilenga kuzungumzia mafanikio katika sekta ya nishati pamoja na maendeleo ya mradi huo mkubwa wa kuzalisha umeme.
“Wizara hii, kupitia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, inatekeleza miradi mikubwa inayowanufaisha Watanzania kwa kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha,” alisema Msigwa.
Ameeleza kuwa mradi wa bwawa la Julius Nyerere unajumuisha manufaa makuu matatu: uzalishaji wa umeme, kilimo cha umwagiliaji, na uvuvi wa kisasa, hivyo kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo kwa maendeleo ya taifa.




Mradi huo ulianza kujengwa mwaka 2019 kwa gharama ya shilingi trilioni 6.558 na umefikia asilimia 99.8 ya utekelezaji. Tayari mashine nane kati ya tisa zimekamilika na zimeingiza megawati 1,880 kwenye Gridi ya Taifa.
Msigwa alisisitiza kuwa mashine ya tisa, ambayo ni ya mwisho, imefikia asilimia 98 ya utekelezaji, huku majaribio ya awali yakitarajiwa kuanza Februari 25. Ifikapo Machi 10, mashine hiyo itaingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa, hivyo kukamilisha uzalishaji wa megawati 2,115.
Katika hatua nyingine, Msigwa amewataka Watanzania kujivunia mradi wa Julius Nyerere, akisisitiza kuwa ni moja ya miradi mikubwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.
