Mtibwa Sugar imeendelea kuimarisha nafasi yake ya kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya TMA kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro. Ushindi huo umeifanya timu hiyo kufikisha pointi 60, ikihitaji pointi 11 pekee ili kufikia 71, idadi ambayo haiwezi kufikiwa na timu nyingine.

Ikiwa na michezo mitano iliyosalia, Mtibwa inahitaji kushinda angalau minne ili kupanda moja kwa moja bila kupitia mchujo. Hata wapinzani wao wa karibu, Mbeya City na Stand United, wakishinda michezo yao yote sita, watamaliza na pointi 70 pekee.
Katika mchezo huo, Fredrick Magata alifunga mabao mawili dakika ya 3 na 15, huku Omari Marungu akihitimisha ushindi dakika ya 32. Magata alisisitiza dhamira ya timu kurejea Ligi Kuu na kuwaomba mashabiki waendelee kuwapa sapoti.