MUHAS Kuandaa Kongamano Kumuenzi Hayati Ali Hassan Mwinyi

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kinatarajia kuandaa kongamano maalum kwa heshima ya Mkuu wake wa kwanza na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi.

Tukio hili la kihistoria litafanyika tarehe 28 Februari 2025 katika Kampasi ya Mloganzila, likilenga kutambua mchango wake mkubwa katika sekta ya elimu, afya, na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Shughuli Muhimu za Kongamano:

  1. Uzinduzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Ali Hassan Mwinyi (AHMMEF)
    Mfuko huu unalenga kusaidia maendeleo endelevu ya elimu na tafiti chuoni, ukitoa msaada wa kifedha kwa miradi bunifu, programu za kitaaluma, na ustawi wa wanafunzi na wanataaluma.
  2. Uzinduzi wa Kongamano la Kila Mwaka la Ali Hassan Mwinyi
    Kongamano hili litakutanisha wataalamu wa sekta ya afya na elimu kujadili maendeleo na changamoto katika sekta hizo. Pia, kutakuwa na hotuba kuu na mijadala yenye lengo la kuimarisha mifumo ya afya na elimu nchini.
  3. Kurejesha Vazi Rasmi la Mkuu wa Kwanza wa Chuo kwa Familia
    Kwa heshima ya Hayati Mwinyi, MUHAS itamkabidhi familia yake vazi rasmi la Mkuu wa Chuo alilolivaa wakati wa mahafali, kama kumbukumbu ya mchango wake katika maendeleo ya elimu.
  4. Maonyesho ya Afya na Elimu
    Yataonesha mafanikio katika sekta ya afya na elimu, yakiwemo tafiti mpya, ubunifu wa kiteknolojia, na juhudi za MUHAS kuboresha huduma za afya. Washiriki pia watapata fursa ya kupima afya zao bure.
  5. Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ndaki ya Tiba
    Kongamano litahitimishwa kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ndaki ya Tiba na Shule ya Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), hatua itakayopanua miundombinu ya Chuo na kuongeza ubora wa mafunzo kwa wanafunzi wa taaluma ya afya.

Kambi Maalum ya Huduma za Afya (26-27 Februari 2025)
Kabla ya kongamano, MUHAS itaendesha kambi maalum ya afya kwa wananchi katika Kampasi ya Mloganzila, ambapo huduma za uchunguzi wa magonjwa kama macho, masikio, pua, koo, meno, saratani, homa ya ini, na tezi dume zitatolewa bure. Pia, kutatolewa elimu kuhusu matumizi ya dawa, magonjwa ya kuambukiza, lishe bora, na ubunifu wa vifaa tiba.

Tukio hili litakuwa fursa muhimu kwa kizazi cha sasa na kijacho kuthamini na kuendeleza maono ya Hayati Ali Hassan Mwinyi katika sekta ya elimu na afya kwa maendeleo ya Taifa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *