Nabii Edmund aonya Watanzania kuepuka machafuko kuelekea Uchaguzi Mkuu

Watanzania wametakiwa kuepuka mashinikizo ya kuhatarisha hali ya usalama wa nchi, yakiwamo maandamano wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Rai hiyo imetolewa na Nabii wa Kanisa la Heavenly Image Manifest (HIM), Nabii Edmund Mystic, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, kuhusu Mkesha mkubwa wa kuliombea Taifa, Rais Samia na uchaguzi mkuu ujao.

Mkesha huo unaotarajia kufanyika Februari 28, mwaka huu, katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, utakaohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa.

“Tumeona mwaka jana kwa habari ya Kenya kulivyotokea machafuko na watumishi wa Mungu walihubiri hivyo hivyo, tunaposikia unabii umetolewa na Mtumishi wa Mungu tusiutweze unabii huo. Hali ya usalama wa Taifa letu ni wetu sote Watanzania kuepuka misukumo ya kulichafua Taifa na sisi viongozi wa dini kusimama kuliombea Taifa,”amesisitiza.

Amewataka pia wagombea wa nafasi za uchaguzi kutotegemea waganga wa kienyeji katika uchaguzi mkuu kwasababu kwenye biblia imeandikwa amelaaniwa yule amtegemeae mwanadamu ni vema kumtegemea Mungu.

“Msimtegemee mganga wa kienyeji kumekuwa na kitu ambacho watu hawakifahamu mganga wa kienyeji anamsaidia mwanasiasa kushinda kwa sababu ya kitu kinaitwa kusimamisha madhabahu ya rohoni,”alisema.

Aidha, amesema wanasiasa watakaogombea wanapaswa kuzingatia uchaguzi unaosimamia haki na sheria ambazo zimeweka nchini.

“Ifike mahali kupata uchaguzi ambao umenyooka na kuwa na uchaguzi huru na wa haki ambaye ni yule Mungu amemkusudia ndiye asimamia na kukaa katika nafasi yake,”amesisitiza Nabii Edmund.

Kuhusu mkesha huo, amesema kanisa lina nafasi ya kulibeba Taifa kwa namna moja na nyingine kwa kufanya maombi, hivyo kupitia maombi hayo yatahusisha pia kumwombea Rais Samia kwasababu yeye ni mtawala na amebeba hatima kubwa ya Watanzania.

Amesema hawawezi kuombea serikali wanayoitazamia kwenye uchaguzi ujao pasipo kuanza na serikali iliyopo madarakani hivyo ni lazima kumwombea Rais Samia ambaye Mungu alimuweka kwenye kiti cha Urais.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *