Matarajio ya Neymar kuelekea Kombe la Dunia lijalo yalipungua zaidi baada ya kushindwa kuonesha kiwango bora kwa Santos katika sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Corinthians katika mechi ya ligi Kuu ya Brazil, Jumapili.
Ulikuwa mchezo wa mwisho wa Neymar kabla ya kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti kutangaza kikosi chake kwa michezo miwili muhimu ya kirafiki jana, na alisema baada ya mchezo huo kwamba, haijalishi kama anataka sana kuwa na timu ya taifa, kwani uamuzi haupo juu yake.
“Natamani kurudi kwenye timu ya taifa na kucheza Kombe la Dunia, lakini hilo si juu yangu,” alisema Neymar akiwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo huo.
“Iwe niko huko au la, nitashangilia Brazil kila wakati.”
Neymar ndiye mfungaji bora wa wakati wote wa Brazil akiwa na mabao 79.
Mechi za Brazil dhidi ya Ufaransa na Croatia nchini Marekani, nazo zitakuwa michezo miwili ya mwisho kabla ya Ancelotti kutangaza kikosi chake cha mwisho Mei kwa ajili ya Kombe la Dunia, litakaloanza Juni 11 hadi Julai 19.
CHANZO: ESPN




