Wakati timu nyingine zikiwa mapumzikoni kutokana na kusimama kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, Pamba Jiji imerejea kambini kujiandaa na mechi nne za mwisho za msimu huu kwa lengo la kuepuka kushuka daraja.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Mathias Wandiba, amesema baada ya mapumziko ya siku nne, kikosi kimeanza mazoezi kwa ajili ya kuwaweka wachezaji kwenye hali ya utimamu wa mwili kabla ya kuanza mafunzo ya kiufundi.
Wandiba amesema lengo lao siyo tu kubaki Ligi Kuu, bali hata kuepuka mechi za mchujo za play-off ambazo zinaweza kuwa hatari. Ameeleza kuwa timu imejifunza kutokana na mapungufu ya mechi zilizopita, hivyo wanajipanga kuhakikisha wanapata ushindi kwenye kila mchezo ili kujihakikishia nafasi salama.
Kwa sasa, Pamba Jiji ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 27, ikisalia na mechi nne dhidi ya Simba (Mei 8), KenGold (Mei 13), JKT Tanzania (Mei 21), na KMC (Mei 25), michezo yote ikiwa na umuhimu mkubwa kwa hatma ya timu hiyo msimu huu.
Kwa mujibu wa benchi la ufundi, ushindi dhidi ya angalau timu tatu kati ya hizo unaweza kuwaokoa moja kwa moja bila kuingia play-off, hivyo kila mchezo utakuwa kama fainali kwao.