Katika ishara ya kina ya unyenyekevu na maisha ya kujitoa kwa Kristo, Baba Mtakatifu Francis ameidhinisha mpango wa mazishi yake kuwa wa kawaida, usio na fahari, kinyume na utaratibu wa muda mrefu wa Kanisa Katoliki kwa mapapa waliomtangulia.

Mazishi ya Mapapa kwa kawaida ni tukio la heshima ya juu, likihusisha taratibu za kifalme na ishara nyingi za heshima kwa kiongozi mkuu wa Kanisa la Kristo duniani. Hata hivyo, Papa Francis, aliyefahamika tangu mwanzo wa upapa wake kwa kuishi maisha ya unyenyekevu, amechagua kufa kama alivyokuwa akiishi – kwa unyenyekevu na utulivu wa kiroho.
Badala ya kuzikwa katika majeneza matatu ya kifahari kama ilivyozoeleka – ya mti wa cypress, risasi (lead), na mwaloni (oak) – Baba Mtakatifu ameagiza atazikwe katika jeneza rahisi la mbao, lililowekwa ndani ya bati la zinki. Ni ishara ya kuonesha kuwa mbele za Mungu, si mali wala vyeo vinavyotupa heshima, bali ni moyo mnyenyekevu na uliopokea neema.
Kadhalika, ameondoa utamaduni wa kuweka mwili wake juu ya catafalque ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kwa watu kuuaga hadharani. Badala yake, waamini wataalikwa kutoa heshima zao za mwisho mbele ya jeneza lake lililofunguliwa juu, ishara ya kuwa kiongozi wao aliishi maisha ya uwazi, karibu na watu wake, na sasa anawakaribisha kumwombea katika safari yake ya mwisho kuelekea uzima wa milele.
Katika hatua ya ajabu na ya kipekee, Papa Francis pia ameamua kuzikwa nje ya mipaka ya Vatican – jambo ambalo halijawahi kutokea kwa zaidi ya karne moja. Atazikwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Major (Basilica di Santa Maria Maggiore), moja ya makanisa ya kipapa yenye hadhi ya juu kabisa jijini Roma. Kanisa hili lina umuhimu wa pekee kwake, kwani mara zote alikuwa akienda kusali hapo kabla ya safari na baada ya kurudi, akiwaweka watu wa Mungu mikononi mwa Mama Yetu Bikira Maria.
Kwa uamuzi huu wa kiroho na wa pekee, Baba Mtakatifu Francis anazidi kuwa mwanga wa unyenyekevu kwa dunia nzima. Anaendelea kufundisha, hata katika kifo, kwamba wito wa Kikristo ni wa maisha ya kujitoa, ya kutumikia, na ya kujiweka katika mikono ya Mungu kwa imani na matumaini.
Requiescat in pace, Servus Dei. Bwana amjalie uzima wa milele, na mwanga wa milele umwangazie. Amina.